Hakimu Afikishwa Mahakamani kwa Rushwa
Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Magomeni, Omary Abdallah na mwenzake, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka manne likiwamo la kuomba na kupokea rushwa.
Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi, Respicius Mwijage, Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa(Takukuru), Emanuel Jacob alimtaja mshtakiwa mwingine kuwa ni George Barongo ambaye ni mfanyabiashara.
Alidai kuwa, kati ya January na Februari 12/ 2017, Omary akiwa mwajiriwa wa Mahakama ya Mwanzo Kinondoni aliomba rushwa ya Sh 205,000 kutoka kwa Agnes Nyenza kwa ajili ya kumsaidia kwenye kesi yake ya mirathi ya namba 570/2016 ambayo ilikuwa mbele yake.
Alidai, shtaka la pili linalomkabili hakimu hiyo pia anadaiwa kupokea rushwa ya kiasi hicho cha fedha Kutoka kwa Nyenza ili aweze kumsaidia katika kesi hiyo.
Alidai kati ya Februari na Machi mwaka huu, jijini Dar es salaam, Hakimu Omary akiwa na mfanyabiashara Barongo waliomba rushwa ya Sh 1,000,000 kutoka kwa Nyenza kwa ajili ya kumsaidia katika kesi hiyo ya mirathi.
Alidai washtakiwa hao katika siku hiyo kwa pamoja walipokea rushwa ya Sh 500,000 kwa ajili ya kumsaidia Agnes Nyenza kwenye kesi yake ya mirathi iiyopo mbele ya hakimu Omary Mohammed wa Mahakama ya Mwanzo Magomeni.
Wakili Jacob alidai, upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hata hivyo washtakiwa hao wamekana mashtaka hayo na Hakimu Mwijage aliwataka washtakiwa hao kila mmoja kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini bondi ya Sh milioni 10. Washtakiwa hao walikidhi masharti ya dhamana na kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 4 mwaka huu.