WANAFUNZI WAJAWAZITO 50 KUFIKISHWA MAHAKAMANI RUKWA
KATIKA kuhakikisha anakomesha tatizo la ujauzito kwa wanafunzi, Mkuu wa
Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, Said Mtanda ameliagiza Jeshi la Polisi
kuhakikisha ndani ya siku saba inazifikisha mahakamani kesi 50 za
wanafunzi waliopewa ujauzito wilayani humo.
Amesisitiza kuwa, wasichana waliobeba ujauzito lazima washitakiwe ili
waweze kuwataja wanaume waliohusika. Aidha, amewapa siku saba watendaji
wa vijiji na kata kuhakikisha wazazi wa watoto 200 ambao hawajaripoti
shuleni kuanza masomo ya kidato cha kwanza mwaka huu, wanakamatwa na
kufikishwa kortini.
Alitoa maagizo hayo wakati wa kikao cha baraza la madiwani wa wilaya ya
Nkasi kilichoketi jana mjini Namanyere yalipo makao makuu ya wilaya ya
Nkasi. “Hali hii haiwezi kuvumilika hapa mjini Namanyere peke yake kuna
zaidi ya wasichana 30 ambao wamekatiza masomo yao baada ya kupatiwa
ujauzito huku katika Kituo cha Polisi cha wilaya ya Nkasi kuna mashauri
ya wanafunzi wa kike 50 ambao wamepewa ujauzito, lakini bado
hayajafikishwa mahakamani.
“Nasema sio kazi ya polisi kusuluhisha kesi za wanafunzi waliopewa
ujauzito , tutakitafiti kituo hiki cha polisi maana zipo taarifa
kinachofanyika pale wana bargain (jadiliana ili kumaliza kesi kienyeji)
na unasikia mtuhumiwa ametoroka.
Sasa, naagiza kesi zote hizo zifikishwe mahakamani ndani ya siku saba,”
alisema. Mkuu huyo wa wilaya ambaye ni mbunge wa zamani wa Jimbo la
Nchinga mkoani Lindi, pia ameyaagiza mabaraza ya kata yawe yamemaliza
kusikiliza mashauri ya kesi za mimba kwa wanafunzi ndani ya siku saba na
hatua zichukuliwe.
Aliwashangaa madiwani wa halmashauri hiyo katika taarifa zao
walizowasilisha kwani hazikuonesha idadi ya wanafunzi waliopewa ujauzito
wala wale ambao hawajaripoti kuanza kidato cha kwanza katika shule za
umma tangu zifunguliwe mapema mwaka huu .
“Leo mkiulizwa katika baraza hili mna maazimio yapi hakuna katika
mijadala yenu kinachosikika ni taarifa miongozo na kanuni,” alisema.
Wakichangia baadhi ya madiwani waliishauri Serikali iwapatie semina
elekezi watendaji wa mabaraza ya kata ili waweze kutekeleza majukumu yao
kwa ufanisi.
IMEANDIKWA NA PETY SIYAME - HABARILEO NKASI