Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto imeahidi kuajiri watumishi wa idara ya afya ili kujaza nafasi
zilizoachwa wazi na watumishi ambao wameondolewa katika utumishi wa umma
kwa kukosa sifa ya kuwa na vyeti halisi baada ya zoezi la uhakiki wa
vyeti nchini.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu
ameyasema hayo jana wakati wa maadhimsho ya Siku ya Wauguzi Duniani
ambapo kitaifa imefanyika katika hospitali ya St. Gasper, Itigi Wilaya
ya Manyoni Mkoani Singida.
Waziri Ummy amesema serikali inatambua mzigo mkubwa wa majukumu kutokana
na uhaba wa wauguzi ambao umesababishwa na baadhi yao kuondolewa katika
utumishi kwa kukosa vyeti halisi na hivyo imetenga bajeti ya kuajiri
wauguzi wa kutosha nchini huku akiahidi kutoa kipaumbele kwa mkoa wa
Singida.
“Kuna baadhi ya Zahanati na vituo vya afya vimefungwa kwa kutokana na
sakata la vyeti feki, lakini pia tunatambua kuwa wauguzi hamtoshi na
hivyo kupelekea muuguzi mmoja kutoa huduma kwa wagonjwa wengi, hali hii
inapunguza ufanisi wenu na kuwanyima haki ya kupumzika”,ameongeza Waziri
Ummy.
Aidha ameagiza waajiri wa utumishi wa umma na hasa halmashauri zote
nchini kupeleka maombi ya watumishi wa kada za afya ili wizara iweze
kutangaza nafasi hizo zijazwe na watanzania wenye sifa huku akisisitiza
kuwa nia ya serikali ya awamu ya tano ni kuboresha huduma za afya kwa
wananchi.
“Serikali imegawa vitanda 25 vya wagonjwa, magoro 25 na mashuka kwa kila
halmashauri nchini huku bajeti ya wizara ya afya ikipanda kutoa
trilioni 1.9 mwaka jana hadi trilioni 2.2 kwa mwaka wa fedha 2017/18,
bajeti hii itasaidia kupambana na changamoto za sekta ya afya nchini nah
ii ni ishara kuwa serikali imedhamiria kuimarisha afya za watanzania”
amefafanua Waziri Ummy.
Kwa upande wake Rais wa Chama cha Wauguzi Tanzania Pulo Magesa amewataka
wauguzi kuto muangusha waziri wao wa Afya kwa kuwa amekua mstari wa
mbele kuhakikisha wauguzi na watumishi wote wa Sekta ya Afya Nchini
wanafanya kazi katika mazingira yanayoridhisha.
Magesa amesema serikali inaweka mazingira mazuri kwa kutenga bajeti ya
kutosha ila ufanisi wake utaonekana endapo watumsihi wa sekta ya afya
hasa wauguzi ambao ndio muhimili wa vituo vya huduma za afya mfano
hospitali, zahanati na vituo vya afya watazingatia misingi ya uadilifu,
upendo na weledi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amesema wauguzi
wanaweza kupunguziwa mzigo wa kupata wagonjwa wengi hasa kwa magonjwa
yanayozuilika endapo kutaanzishwa mfumo wa utoaji wa huduma za uuguzi
kwa ngazi za kaya ambapo kila mwanafamilia atapewa elimu ya kuzuia
baadhi ya magonjwa.
Dkt. Nchimbi amesema mfumo huo wa uuguzi kaya uendeshwe mpaka kwenye
taasisi za elimu hasa shule za msingi na sekondari ili jamii iweze
kuzuia kwa kiwango magonjwa yote yanayozuilika na hivyo kupunguza
msongamano wa wagonjwa .
Aidha amemshukuru Waziri Ummy kwa kuunga mkono wazo hilo na kukubali
kuanza kulifanyia kazi huku akiahidi kutoa ushirikiano kwa kuwa mkoa wa
Singida utatumika na sehemu ya utafiti wa mfumo huo ili kufahamu ufanisi
wake
Maadhimisho Siku ya Wauguzi Duniani ni kukumbuka ya muasisi wa taaluma
ya uuguzi Bi.Florence Nightngale aliyezaliwa Mei 12 mwaka 1820. Wakati
wa sherehe hizi huwa mishumaa inawashwa kama ishara ya upendo na
utumishi bora moyoni mwa muuguzi. Muasisi huyu ndiye aliyefungua chuo
cha kwanza cha uuguzi nchini Uingereza.
Bi Florence alianza kutoa huduma ya afya mwaka 1844 na mwaka mmoja
baadaye kulitokea vita na yeye akawa anahudumia majeruhi kwa kutumia
mishumaa nyakati za usiku kwa vile hapakuwepo na nishati yoyote wakati
huo. Bi Florence kwa huduma yake hiyo ya kutibu majeruhi wa vita aliweze
kupunza vifo kutoa asilimia 42 hadi asilimia mbili (2).
Wauguzi waliokuwepo kwenye maadhimisho hayo kutoka mikoa mbalimbali
nchini walirudia kiapo chao cha uuguzi ambacho sehemu mojawapo inasema
“Naapa mbele ya Mungu na mbele ya mhadhara huu, kuendesha maisha yangu
na kutekeleza wajibu wangu wa kazi kwa uaminifu. Sitafanya vitendo vyo
vyote vile vilivyo viovu na sitochukua au kutoa dawa ye yote ile
ninayoifahamu kuwa ina madhara”.
Awali wauguzi, viongozi mbalimbali wa serikali na madhehebu ya dini
pamoja na wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo walisimama kwa dakika
moja kuwakumbuka na kuwaombea wanafunzi 32, walimu wawili na dereva wa
shule ya Lucy city ya Mjini Arusha waliopoteza maisha yao kwenye ajali
mbaya ya gari iliyotokea hivi karibuni.