SENSA YA WAFANYAKAZI WA NYUMBANI KUFANYIKA MKOANI MWANZA.
Jackline Ngalo ambaye
ni Mwanasheria wa shirika la kutetea Haki za watoto wafanyakazi wa
nyumbani nchini, WOTESAWA, akizungumza na Lake Fm, baada ya semina kwa
viongozi wa serikali za Kata/Mitaa pamoja na wadau wengine wa maendeleo
katika wilaya za Ilemela na Nyamagana mkoani Mwanza ili kuwajengea uwezo
wa kutetea haki za watoto wafanyakazi wa nyumbani katika maeneo yao.
Na Binagi Media Group
Semina kwa viongozi wa
serikali za Mitaa pamoja na wadau wengine wa maendeleo katika wilaya za
Ilemela na Nyamagana mkoani Mwanza ikiendelea Jijini Mwanza
Semina hiyo imeandaliwa na shirika la WOTESAWA kwa siku tatu tangu Mei 09 hadi leo Mei 11,2017
Washiriki wa semina hiyo wakimsikiliza mwanahabari Nashon Kenedy, wakati akichangia mada kwenye semina hiyo
Wadau wa
Maendeleo mkoani Mwanza wameidhinisha mikakati mbalimbali ikiwemo
kufanya sensa ya watoto wafanyakazi wa nyumbani na utungwaji wa sheria
ndogo ndogo za kuwalinda watoto, lengo likiwa ni kusaidia mapambano
dhidi ya ukatili kwa watoto hao.
Wamefikia
makubaliano hayo leo kwenye kilele cha mafunzo ya siku tatu kwa viongozi
wa serikali za mitaa kutoka Wilaya za Nyamagana na Ilemela
yaliyoandaliwa na Shirika la kutetea Haki za watoto wafanyakazi wa
nyumbani la WOTESAWA lililopo Jijini Mwanza.
Akizungumzia
mikakati hiyo, Jackline Ngalo ambaye ni Mwanasheria wa shirika la
WOTESAWA amebainisha kwamba, mikakati hiyo itasaidia kuwalinda watoto
wafanyakazi wa nyumbani ikiwemo kuwanusuru na utumikishwaji wa kazi
nzito huku wakilipwa ujira mdogo.
Wadau
walioafiki mikakati hiyo ni Madiwani, Watendaji wa Kata, Wenyeviti wa
Mitaa, Maafisa Ustawi na Maendeleo ya Jamii ambapo wameongeza kwamba
mafunzo hayo yatawasaidia kuielimisha jamii kupitia mikutano ya hadhara
ili kuepukana na ukatili kwa watoto hususani wafanyakazi wa nyumbani.
Baadhi ya
watoto wamekuwa wakikosa fursa ya kusoma kutokana na kuajiriwa katika
kazi za nyumbani kinyume na sheria huku wakilipwa ujira mdogo tofauti na
waraka wamishahara wa mwaka 2013 unavyoelekeza.
Waraka huo
unaelekeza kwamba mfanyakazi wa kazi za nyumbani anapaswa kulipwa
kiwango cha chini cha mshahara ambacho ni shingili 150,000 iwapo mwajiri
ni balozi ama mfanyabiashara mkubwa, elfu 80,000 ikiwa mwajiriwa haishi
kwenye nyumba ya mwajiri wake, elfu 40,000 ikiwa mwajiriwa anaishi
kwenye nyumba ya mwajiri wake na shilingi 130,000 ikiwa mwajiri ni raia
wa kigeni.