SAKATA LA KATIBU MKUU WA CCM KINANA KUDAIWA KUFICHWA LAZUA BALAA BUNGENI DODOMA
Kauli aliyoitoa bungeni juzi usiku mbunge wa Arusha Mjini (Chadema),
Godbless Lema kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana amefichwa
ilisababisha mawaziri wawili wa sasa na mmoja wa zamani wamkomalie
kuifuta.
Bunge lilikuwa likijadili Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Awali, Lema alisema ameona kwenye mitandao juu ya Kinana kufichwa na
kupaza sauti akitaka kumtetea akiwa kama Waziri Kivuli wa Mambo ya
Ndani.
Hata hivyo, kauli hiyo ilimsimamisha Waziri wa Tamisemi, George
Simbachawene akitumia kanuni ya 64 (2) ambayo alisema inatoa nafasi
kukumbusha Bunge kwamba kuna kanuni inayovunjwa.
“Mbunge anayezungumza anasema jambo ambalo hana uhakika nalo, linatia
mashaka, sidhani kama ana uhakika kwamba Kinana amefichwa.
Alithibitishie Bunge hili na kama hawezi kuthibitisha, kupitia kanuni ya
72 (2) nakuomba Mwenyekiti umtake afute maneno hayo,” alisema
Simbachawene.
Ufafanuzi huo ulimuinua kitini Tundu Lissu na kusema Simbachawene hajui atendalo, Mungu amsamehe.
“Kanuni ya 72 (2) inasema mbunge atakayekiuka utaratibu uliowekwa na
kanuni hizi anaweza kutakiwa na Spika hapohapo afuate utaratibu au
mbunge atasimama kwa kutumia utaratibu huo na kutaja kanuni
iliyokiukwa,” alisema Lissu.
Baada ya maelezo hayo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenister
Mhagama ambaye ni mnadhimu mkuu wa Serikali aliweka msisitizo kwenye
kanuni ya 64 (1) (a) ambayo inakataza mbunge kutotoa taarifa ambazo
hazina ukweli.
“Naomba nimthibitishie mheshimiwa Lema kwamba Kinana tumezungumza naye
wakati wa maadhimisho ya Muungano, wakati wa maadhimisho ya Mei Mosi.
Kinana ametoka kwenye matibabu na sasa anapumzika nyumbani kwake.
Alipomaliza kuzungumza Jenister aliinuka Mbunge wa Newala (CCM), George
Mkuchika ambaye aliwahi kuwa waziri wa wizara mbalimbali katika Serikali
ya Awamu ya Nne na kuomba mwongozo wa mwenyekiti kuwa tangu Lema aanze
kuchangia hakuwa anazungumzia jambo lililoko mezani, yaani bajeti ya
wizara ya habari.
“Mheshimiwa Lema tangu ameanza hakuzungumza habari zozote kuhusu wizara.
Mimi kwa umri huu hata ukinizomea siachi kuzungumza. Mheshimiwa
Mwenyekiti naomba muongozo wako kuhusu kanuni ya 64 (b) inayosema mbunge
hatazungumzia jambo nje ya mjadala.
Akitoa mwongozo wake Mwenyekiti wa Bunge, Azzan Zungu alisema kwa mujibu
wa kanuni hizi 68 (10) Spika ndiye mwenye uamuzi wa mwisho kuhusu
masuala yote ya kanuni, kwa hiyo akamtaka Lema afute maneno hayo na Lema
aliyafuta akisema anafanya hivyo kwa kuwa waziri amemhakikisha kwamba
Kinana hajatekwa.