Waziri
wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt Harisson Mwakyembe
(katikati) akiwa katika picha ya pamoja
na baadhi ya viongozi wa Riadha na Washindi wa mashindano ya Riadha kwa vijana
walio chini ya miaka 18 yaliyoshirikisha nchi saba za Afrika Mashariki na
Kati leo Jijini Dar es Salaam.
Picha/Habari na Shamimu Nyaki
Mchezo
wa Riadha umekuwa na mchango mkubwa katika kukuza na kuimarisha ushirikiano
baina ya Afrika Mashariki na Kati kwa kuwa nchi wanachama wamekuwa wakifanya mashindano
mbalimbali yaliyochangia kuleta ukaribu miongoni mwa Jumuiya hiyo.
Hayo
yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari
Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harisson Mwakyembe alipokuwa akifungua
mashindano ya Riadha kwa vijana wenye umri chini ya Miaka 18 yaliyojumuisha
nchi saba za Afika Mashariki na Kati ambapo ametumia nafasi hiyo kuwahamasisha
vijana wenye vipaji na uwezo wa kufanya riadha kutumia mashindano hayo kama
njia ya kujifunza na kufanya vizuri.
“Mashindano
haya ni mazuri yanatoa hamasa kwenu
vijana kuyatumia kama njia ya kujifunza ili mfanye vizuri kama wanariadha
wengine waliowahi kufanya vizuri na wanaoendelea kufanya vizuri ndani na nje ya
Afrika lakini pia yametuunganisha sisi wana Afrika Mashariki na Kati pamoja na
kuimarisha uhusiano wetu ”Alisema Mhe. Waziri.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Riadha Tanzania Bw.
Filbert Bayi ameeleza kuwa mchezo wa riadha umeanza kurudi katika hadhi yake ya
zamani baada ya vijana wengi kuanza kuupenda na kushiriki mashindano mbalimbali
ya riadha ambayo yamekuwa yakiwapatia
mafanikio.
“Hivi
sasa riadha imeanza kupendwa vijana wengi wanajitokeza katika mchezo huu na mashindano mbalimbali wakiwa na ari kubwa ya
kutamani kufika mbali tunachotakiwa kufanya ni kuwaunga mkono,” Aliongeza Bw
Filbert.
Naye
Mshiriki wa Mshindi wa Mita 100 kutoka Tanzania Bi Keflin Kipili amesema kuwa
riadha ni mchezo unaoleta mafaniko hivi sasa Ulimwenguni kwa vijana kama yeye
hivyo ni vyema kwa vijana kuumia vipaji walivyonavyo anatumia kupata mafanikio
zaidi.
Katika
mashindano hayo Nchi ya Kenya imekuwa kinara kwa kuibuka kidedea kwa kushinda
medali tatu za dhahabu katika mbio za mita 800 Wasichana na Wavulana,pamoja na
mita 3000 Wavulana huku Tanzania ikiibuka kidedea katika mbio za mita 100
Wasichana, kubadilishana vijiti (relay) Wasichana na Wavulana.
Mashindano
hayo ya siku mbili yanafanyika Jijini Dar es Salaam yanahusisha Nchi saba za
Afrika mashariki na Kati ambazo ni Tanzania ambao ndio wenyeji, Kenya,Zanzibar,Somalia,Sudan
Kusini na Eritrea.
|