PAMOJA NA KUTEREMKA DARAJA, JKT RUVU WATOA AHADI HII...
Baada ya JKT Ruvu kuchezea kichapo cha
mabao 2-1 kutoka kwa Toto Africans ya Mwanza, kocha msaidizi wa timu
hiyo, Azishi Kondo, amesalimu amri na kuongea kwa unyonge kwamba
anasubiri kuona timu mbili zikiungana na timu yake kushuka daraja msimu
huu.
JKT Ruvu baada ya kichapo hicho,
imeshuka daraja ikiwa na pointi 23 huku ikibakiwa na michezo miwili
ambayo hata ikishinda haiwezi kuwaokoa na janga hilo.
Kondo alisema kuwa japokuwa wameshashuka
daraja, lakini hawatakubali kufungwa katika mechi zao mbili zilizobaki
dhidi ya Majimaji na Ndanda FC.
“Sisi tushashuka daraja na msimu ujao
tutacheza Ligi Daraja la Kwanza, kwa sasa tunasubiri kuona ni timu gani
tutaungana nazo, lakini japokuwa tumeshashuka, hatutakubali kufungwa
kwenye mechi zetu mbili zilizobaki.
“Sasa hivi tunajipanga kucheza na
Majimaji katika uwanja wetu wa nyumbani wa Mkwakwani uliopo Tanga, kisha
tunamalizia na Ndanda kule kwao kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona na
mechi zote tunataka kuibuka na ushindi,” alisema Kondo.
SOURCE: CHAMPIONI