Majeruhi wa ajali ya gari iliyohusisha
vifo 35 vya wanafunzi, walimu pamoja na dereva wa shule ya msingi Luck
Vicent wilayani Karatu, wamesafirishwa jana kwenda Marekani kwa ajili
ya matibabu zaidi .
Akizungumza katika uwanja wa ndege wa
Kia, Mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo alisema kuwa majeruhi hao
wanasafirishwa na ndege ya Shirika la Samaritan Purse ili kuwawezesha
kupatiwa huduma za matibabu zaidi ambazo zitaweza kurejeshea afya zao.
Gambo alisema kuwa Serikali imejitahidi
kwa hali na mali kuhakikisha kuwa wamewafariji wale wote waliofikwa na
msiba na hata kuhakikisha kuwa majeruhi waliobaki wanapatiwa huduma
ambazo zitaweza kunusuru maisha yao.
Gambo aliwataka wakazi wa jiji la Arusha
na viunga vyake kuacha kutumia mitandao ya kijamii vibaya kwa kuwa
inakwamisha huduma za kijamii kwa ajili ya kuchanganya na shuguli za
kisiasa.
"Naombeni sana wana Arusha muache
kutumia mitandao ya kijamii vibaya kwani hii mitandao imepotosha sana
mambo mengi imehusisha huduma za kijamii kuwa mambo ya kisiasa hali
ambayo inasababisha hata wanaojitokeza kuchangia maafa haya kuvunjika
moyo kwa ajili ya mambo yaliyoandikwa kwenye mitandao ya hiyo"-alisema
Gambo
Alidai kuwa huduma za kijamii hazipaswi
kuhusishwa na shughuli za kisiasa kwani endapo zitahusishwa zitakwamisha
hata wale wanaoendelea kufariji kushindwa kuendelea na moyo huo.
Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro
Nyalandu ambaye ni mmoja wa waliojitolea kufanikisha safari hiyo
aliwataka Watanzania kuendelea kuombea majeruhi hao ili wapone haraka.
Safari ya majeruhi hao kuelekea Marekani
ilianza saa 5:40 asubuhi wakiambatana na mkuu wa wilaya ya Hai,
Gelasius Gaspa ambaye amemwakilisha mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Meck
Sadiki.