Rai hiyo imetolewa na Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa
Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakati wa uzinduzi wa Mbio za Mwenge
wa Uhuru mwaka 2017 leo katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Mwenge wa Uhuru Mkoani
Katavi na kusema kuwa Uchumi wa viwanda uliodhamiriwa ni ule utakaolifanya
taifa kuzalisha bidhaa bora na zenye ushindani wa soko la kimataifa badala ya
kuwa chanzo cha malighafi na soko la bidhaa za viwanda vya mataifa mengine.
“Tanzania tumeazimia kutoka katika kundi la
uchumi duni na kwenda kwenye ujenzi wa uchumi wa viwanda, Ujenzi na uimarisha wa viwanda nchini ambao utahusisha wadau
mbalimbali wa Maendeleo, wananchi wenyewe, sekta binafsi na Mashirika Mbalimbali ya
Kimataifa yanayo nafasi kubwa hususan katika uwekezaji mkubwa, ukuzaji wa
mitaji, masoko, Teknologia na upatikanaji wa rasimali watu wenye ujuzi
maalum” amesema Mhe. Balozi Iddi.
Aidha Mhe. Balozi Iddi amesema kuwa wananchi wanayo fursa kubwa sana
katika kujenga na kuendeleza viwanda nchini kwani ukuaji wa uchumi wa Viwanda
unaanza kwa jitihada za wananchi wenyewe katika kuanzisha na kuendesha viwanda
vidogo vidogo vinavyoweza kuongeza thamani ya mazao na bidhaa wanazozalisha
kila siku katika maeneo yanayowazunguka.
Akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Katavi Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira, na Walemavu Mhe.
Jenista Mhagama amesema kuwa mbio za mwenge wa uhuru zimekua zikihamasisha amani,
mshikamano, kujenga uzalendo na umoja wa kitaifa kwa kuhamasisha miradi
mbalimbali ya kimaendeleo ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ipo sambamba na
malengo ya serikali ya awamu ya tano ambayo imedhamiria kukuza uchumi wa
viwanda kwa kufufua viwanda vilivyopo kuanzisha viwanda vidogo vidogo, viwanda
vya kati na viwanda vikubwa.
Mwaka huu, ujumbe mkuu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru
unahusu Mkakati wa kukuza Viwanda nchini, chini ya Kauli Mbiu isemayo:- “Shiriki Kukuza Uchumi wa Viwanda kwa
maendeleo ya nchi yetu”. Ujumbe huu utaambatana na msisitizo wa Serikali
kuhusu mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI, Malaria, Dawa za Kulevya na Rushwa.
Mwenge wa Uhuru uliasisiwa na Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1961 ikiwa ni tunu na ishara ya kuwepo
kwa Taifa huru la Tanganyika. Hatua hiyo ilikuwa ni utekelezaji wa ndoto yake
iliyotafsiriwa kwa maneno aliyoyatamka mwaka 1958 kwa wajumbe wa Baraza la
kikoloni la kutunga Sheria na kuyarudia tena mwaka 1959 alipohutubia kikao cha
35 cha Baraza la Umoja wa Mataifa wakati huo akidai Serikali ya madaraka kama
Mbunge mwakilishi pekee wa Tanganyika kwa kusema “Sisi watu wa Tanganyika, tungependa kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya
Mlima Kilimanjaro, umulike ndani na nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale
ambapo hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki na heshima palipo jaa
dharau”.Falsafa hiyo ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ujumbe mkubwa kwa Waingereza kwamba, watu wa
Tanganyika wamechoka kutawaliwa.