Kamanda wa polisi mkoani Pwani,
Boniventure Mushongi,anayehamia mkoa wa Simiyu akizungumzia tukio la
mauaji ya mwenyekiti wa kitongoji cha Kazamoyo huko Rufiji (Picha na
Mwamvua Mwinyi)
MAUAJI kwa viongozi wa vijiji na vitongoji mkoani Pwani hususan wilayani
Rufiji vimeendelea kujitokeza ambapo mwenyekiti wa kitongoji cha
Kazamoyo wilayani Rufiji Hemed Njiwa (45) ameuawa kwa kupigwa risasi.
Kamanda wa polisi mkoa wa Pwani, Boniventure Mushongi ambaye
anahamishiwa mkoa wa Simiyu alisema marehemu aliuawa na watu
wasiojulikana wakati akiwa nyumbani.
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia machi 13 ,eneo la Kifuru kata na tarafa ya Ikwiriri wilayani hapo.
“Marehemu alipigwa risasi kifuani akiwa nyumbani kwa mke wake mdogo
Maimuna Abdallah (36)na alikutwa na jeraha la risasi kwenye mkono wake
wa kushoto”,alisema.
Kamanda Mushongi,alieleza kwamba mtu ama watu aliyehusika na tukio hilo
baada ya kumuua alikimbia kusikojulikana kwa kutumia pikipiki aina ya
boxer ambayo haikuwa na namba za usajili.
Alisema hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa na jeshi la polisi linaendelea
na msako mkali ili kuweza kubaini watu waliohusika na tukio hilo.
Kamanda huyo aliwataka wananchi kuwafichua watu wanaohusika na matukio
ya kuua viongozi wa vijiji na vitongoji kwani hilo linaweka idadi ya
matukio zaidi ya matatu yaliyohusisha viongozi hao.