Serikali imepiga marufuku watu kufunga ndoa bila kuwa na cheti cha kuzaliwa kuanzia Mei Mosi, mwaka huu.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe amesema hayo jana
Machi 16,2017 akiwa katika ziara yake mkoani Morogoro na kuongeza kuwa
serikali imeamua kufanya hivyo ili kupata takwimu sahihi za wananchi
wake zitakazosaidia kupanga mipango ya kimaendeleo sanjari na kuzuia
wageni kuingia kinyemela nchini.
Pamoja na mambo mengine, Dk.Mwakyembe amewataka Wakala wa Usajili wa
vizazi na Vifo (RITA), kuhakikisha inasimamia sheria ya usajili ambapo
amesema kuwa bila kuwa na takwimu sahihi za vizazi na vifo ama ndoa
inasababisha nchi kushindwa kusonga mbele kimaendeleo.
“Wenzetu nchi zilizoendelea suala la usajili wamelipa kipaumbele lakini
sisi bado tuko nyuma, kwa mfano Mkoa wa Morogoro kwa mujibu wa sensa
ya watu na makazi ya mwaka 2012, inaonyesha kuna jumla ya wakazi milioni
2.2, lakini waliosajiliwa na kuwa na vyeti vya kuzaliwa ni asilimia 11
pekee huku wengine wakiwa bado hawasajiliwa,” amesema.
Dk. Mwakyembe pia ametumia nafasi hiyo kuwaonya watendaji wa mahakama
watakaolalamikiwa na wananchi kufanya kazi kinyume na maadili ikiwamo
upokeaji wa rushwa ama kutotenda haki na kutumia mahakama kugeuza kesi
za madai kuwa kesi za jinai.