MAKABURI 22 YA WATU WENYE UALBINO YAFUKULIWA TANZANIA...TAS YAMUOMBA RAIS MAGUFULI KUFANYA KAMA DAWA ZA KULEVYA NA VIROBA
Chama cha watu wenye ualbino Tanzania
(TAS) kimelaani vikali vitendo vya ufukuaji wa makaburi ya watu wenye
ualbino vinavyoendelea kujitokeza nchini hali inayowafanya waishi kwa
hofu kubwa katika nchi yao.
Inaelezwa kuwa tangu kuibuka kwa mauaji
ya watu wenye ualbino mwaka 2007 takribani makaburi 22 nchini Tanzania
yamefukuliwa na watu wasiojulikana.
Chama hicho kimeiomba serikali ya awamu
ya tano inayoongozwa na rais John Pombe Magufuli kuweka mkazo katika
mapambano dhidi ya ukatili wa watu wenye ulemavu wa ngozi kama
ilivyoonesha nguvu za kutosha katika vita ya dawa za kulevya na pombe
aina ya viroba.
Akizungumza juzi kwenye kikao cha
viongozi wa chama watu wenye ualbino kutoka mikoa ya kanda ya Ziwa
ambayo ni Mara,Mwanza na Shinyanga na wanachama wengine Afisa mahusiano
na habari TAS taifa Josephat Torner vitendo vya kufua makaburi ya watu
wenye ualbino yanatishia amani yao
Torner alisema wanaiomba serikali
kuelekeza nguvu katika masuala ya mauaji na ufukuaji wa makaburi ili
kuwafanya watu wenye ualbino waishi kwa amani ndani ya nchi yao.
“Katika suala la mauaji ya watu wenye
ualbino ambao wamekuwa wakiishi kwa hofu tunaomba serikali hata
kuwataja kwa majina wanunuzi hao kama ilivyotokea kwenye masuala ya
vita ya dawa zakulevya na uuzaji bombe aina ya viroba”,alisema
Torner.
Aidha alisema wanalaani kitendo cha
kufukuliwa kwa kaburi la Nelson Msogole (50) aliyekuwa akiishi mji
wa Songwe baada ya kufariki tarehe 28/3/2011 na kaburi lake
kuonekana kufukuliwa tarehe 20/3/2017na watu wasiojulikana.
“Matukio haya yanaendeshwa kwa usiri
hivyo tunahoji kwanini imeshindikana ikiwa kwenye dawa za kulevya
wameweza kutaja na kumepiga hatua?”,alihoji Torner.
Alisema Tangu kuanze kuibuka mauaji ya
watu wenye ualbino mwaka 2007 makaburi 22 nchini yamekwisha fukuliwa
katika mikoa ya Mbeya ,Tabora,Mwanza,Mara ,Kagera,Rukwa, na Shinyanga.
Aliiomba serikali ya awamu ya tano
iweke mikakati ya uelewa kwenye jamii kwani huenda hawana uelewa na
watuhumiwa wakibainika waadhibiwe kwa mujibu wa sheria.
“Hiki ni kipimo cha serikali ya awamu
ya tano kwa sauti ya wanyonge kwani kuna baadhi ya watu wanaishi
kwenye nchi yao kwa hofu na unyonge na kuondolewa utu wao hivyo tuna
imani serikali itaweka nguvu kubwa kuliko kipindi cha nyuma”,aliongeza Torner.
Naye Mwenyekiti wa chama hicho kutoka
mkoani Mwanza Alfredy Kapole alisema mkoa wa Mwanza unaongoza kwa
mauaji ya vifo vya albino zaidi ya 17 vimetokea tangu mwaka 2007
hivyo aliiomba serikali kuweka ulinzi mkubwa kwa watu hao kwani
wanakiuka katiba ya nchi kwani kila mtu anastahili kuishi.
Mwenyekiti wa chama hicho kutoka mkoani
Mara Joseph Sinda alisema kitendo cha kufukua kinawafanya waishi kwa
hofu kubwa na kuitaka serikali ijaribu kuchunguza chanzo chake ni nini
na kuthibiti kama kwenye madawa ya kulevya na pombe aina ya viroba
walivyofanya ili waweze kuishi kwa amani.
Mwanaharakati kutoka mkoani wa
Shinyanga Eunice Zabroni aliiomba serikali wawaimarishie ulinzi na
elimu itolewe kwani wanaishi kwa hofu kwa kukosekana ulinzi imara
kuanzia ngazi ya vitongoji,vijiji kata na wilaya hadi mkoa.
Habari na Kareny Masasy- Malunde1 blog
Katikati ni Afisa mahusiano na habari wa chama cha watu wenye ualbino nchini Tanzania (TAS )Josephat
Torner akizungumza wakati wa kikao cha viongozi na wanachama wa chama
hicho ambapo walilaani vitendo vya ufukuaji wa makaburi ya watu wenye
ualbino.Kulia ni Mwenyekiti TAS mkoa wa Mara Joseph Sinda,kushoto ni mwenyekiti TAS mkoa wa MwanzaAlfred Kapole -Picha zote na Suzy Butondo-Malunde1 blog
Afisa mahusiano na habari wa chama cha watu wenye ualbino nchini Tanzania (TAS )Josephat
Torner ambapo alisema chama hicho kinaiomba serikali ya awamu ya tano
inayoongozwa na rais John Magufuli kuongeza kasi katika mapambano dhidi
ya ukatili wa watu wenye ualbino
Baadhi ya wanachama wa chama cha watu wenye ualbino nchini Tanzania wakiwa katika kikao hicho.
Picha na Suzy Butondo-Malunde1 blog