Makonda ayakana makontena Yaliyoko Bandarini
Utata
umeendelea kuandama umiliki wa makontena 20 yaliyotajwa na Mamlaka ya
Mapato (TRA), kuwa miongoni mwa yale yatakayopigwa mnada kwa kukaa
bandarini muda mrefu, baada ya mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda kukana kuwa sio ya kwake.
Awali,
TRA ilitoa tangazo katika gazeti la Daily News, ikisema mtu aitwaye
Paul Makonda bila kubainisha kama mtajwa ni mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam au la, anamiliki makontena 20 yenye bidhaa mbalimbali zikiwamo
samani katika bandari kavu ya DICD.
Hata
hivyo, akizungumza jana wakati akizindua kamati ya mapendekezo kuhusu
wanawake waliotelekezwa na wenza wao, Makonda alisema hajui chochote na
amesikia habari hizo kwenye magazeti kama walivyozisikia watu wengine.
“Sidhani
kama nahusika na jambo lolote lile na sijui chochote, hilo unalolisema
hata mimi nimesoma kwenye magazeti kama ulivyosoma wewe. Nafikiri
zilikuwa ni habari za jana na leo nimesoma nyingine,” alisema.
Makonda alisema Serikali hufanya kazi zake kwa maandishi na yeye hana nakala yoyote inayohusiana na mzigo huo.
“Sio
suala la kwangu kabisa, nimekusikia wewe kama mimi nilivyosikia jana
(juzi) na ninafikiri tutaendelea kusikia hivyo hivyo na ndio maana
katika hizo habari hakuna sehemu yoyote umeona nimenukuliwa kusema kama
ni mali zangu,” alisema Makonda.
Hata
hivyo, Februari 16, Makonda alikaririwa na gazeti la Serikali la
HabariLeo kuwa alipokea makontena 20 yenye samani zitakazotumika katika
ofisi za walimu zinazoendelea kujengwa ukiwa ni sehemu ya shehena ya
makontena 36.
Ilielezwa
kuwa samani hizo za ofisini zilizokuwa na thamani ya Sh2 bilioni,
zilitolewa na Watanzania wanaoishi Marekani wanaojulikana kama Six
Region Diaspora Council.
Mei,
12 kaimu kamishna wa Forodha na Ushuru wa TRA, Ben Asubisye alisema
wamiliki wa mizigo hiyo wanatakiwa kuikomboa ndani ya siku 30 kuanzia
siku hiyo. Katika tangazo hilo lenye orodha ya makontena zaidi ya 800,
jina la Paul Makonda limejitokeza mara 20 akiwa mpokeaji wa makontena 20
yakiwa na bidhaa kadhaa, zikiwamo samani.
Mkurugenzi
wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema juzi
kuwa mamlaka hiyo imetoa notisi ya siku 30 kwa waagizaji wa mizigo
ambayo imekaa bandarini kwa zaidi ya siku 90.
“Tangazo
lililotolewa ni notice (taarifa) kwa wahusika ili wakomboe mizigo yao
ndani ya siku 30. Isipokombolewa itanadiwa. Mizigo hiyo inaweza kuwa ni
ile ambayo haijalipiwa kodi au hata ile iliyolipiwa lakini
haijaondolewa,” alisema.
Alipoulizwa
kama shehena hiyo ni mali binafsi ya Makonda au ya ofisi yake, Kayombo
alisema: “Majina yaliyoandikwa kwenye magazeti ndiyo taarifa za
consignees (wapokeaji) zilizopo kwenye nyaraka.”