IGP Sirro awapa onyo waliopata msamaha wa Rais Magufuli
Mkuu
wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro amewaonya watu waliopata
msamaha wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli wa Aprili 26, 2018 wajichunge
tabia na matendo yao.
IGP
Sirro ametoa onyo hilo jana Mei 24, 2018 mbele ya Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa vituo vya polisi vya kisasa
vya Mburahati, Kiluvya-Gogoni na Mbweni ambavyo vimezinduliwa leo.
"Nia
ya Mheshimiwa Rais Magufuli kuwapa msamaha ilikuwa njema lakini kuna
baadhi ya watu wameitumia vibaya fursa hiyo na hadi sasa watu watano
wamekwishauawa na wananchi.
"Natoa
onyo kwa wote waliopata msamaha na wana nia ya kurejea kwenye matendo
yao maovu, ukitoka gerezani kwa msamaha, maana yake umerekebisha
mwenendo wako na wananchi wanatarajia uwe hivyo, lakini kama ukifanya
vinginevyo, serikali isilaumiwe", amesema IGP Sirro.
Akielezea
kuhusu utendaji wa Jeshi la Polisi, Kamanda Sirro amesema tangu ashike
madaraka hayo, jeshi hilo limewapeleka askari 1,267 kwenye mafunzo ya
medani za kivita na kwamba jeshi hilo liko imara.
"Pia
tumepeleka askari wa upelelezi zaidi ya 1,000 kwenye mafunzo ya ujuzi
na ustadi (skills and knowledge) wa kupeleleza kesi mbalimbali.
"Baada
ya kuwapa mafunzo haya, tunataka kesi za kawaida upelelezi wake uwe
umekamilika ndani ya miezi sita na zile kesi kubwa kubwa upelelezi wake
uwe umekamilika ndani ya miezi 12. Tunataka kuhakikisha haki za
watanzania zinapatikana kwa wakati," amesisitiza Sirro.
Kwa
upande mwingine, Kamanda Sirro alitumia fursa hiyo kumshukuru pia Rais
Magufuli kwa kuwapatia sh. bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za
askari, kutoa kibali cha ajira kwa askari wapya 1,500 na kuwaruhusu
wawapandishe vyeo askari wenye kustahili kuanzia cheo cha Koplo hadi
Naibu Kamishna wa Polisi (DCP).