Waziri Mkuu: Serikali kuimarisha masoko ya mazao
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali inataka kuimarisha masoko ya
mazao yanayolimwa nchini ili kuwawezesha wakulima kupata tija.
Taarifa
iliyotolewa jana Februari 3, 2018 na ofisi ya Waziri Mkuu inaeleza
kuwa ametoa kauli hiyo Januari 2, 2018 wakati akikagua Kampuni ya Soko
la Bidhaa Tanzania (TMX), iliyoanzishwa kwa lengo la kuimarisha masoko.
Amesema
kupitia Wizara ya Kilimo, Serikali imedhamiria kuimarisha masoko ya
mazao yanayolimwa nchini ili kuwawezesha wakulima kujikwamua kiuchumi.
“Kupitia
Wizara ya Kilimo tunataka kuimarisha masoko ya mazao yanayolimwa
nchini. Wakati umefika kwa wakulima nchini kuona tija ya mazao
wanayolima,” amesema.
Ametoa
mfano zao la pamba ambalo wakulima walikuwa wanaingia mikataba na
wanunuzi, mfumo ambao ulikuwa unawanyonya badala ya kuwanufaisha.
Awali, ofisa mtendaji mkuu wa TMX, Godfrey Malekano amemhakikishia Waziri Mkuu kuwa wamejipanga vyema kuanza minada ya mazao.
“Tutaanzia na zao la ufuta mwezi Mei, 2018 na kuendelea na mazao mengine kwa kadiri ya misimu ya mazao hayo ilivyo,” amesema.
Amesema
kufanikiwa kwa soko la bidhaa na mfumo wa stakabadhi ghalani
kunategemea msaada wa Serikali, “Soko la bidhaa la Ethiopia linalotajwa
sana kwa mafanikio limefikia malengo yake kutokana na mkono wa
Serikali.”