Rais Magufuli azindua Kituo cha Mafunzo Maalum ya Kijeshi
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
tarehe 06 Februari, 2018 amezindua Kituo cha Mafunzo Maalum ya Kijeshi
(Comprehensive Training Center – CTC) kilichopo Mapinga katika Wilaya ya
Bagamoyo Mkoani Pwani.
Kituo
hicho kimejengwa kwa msaada kutoka Jeshi la Ukombozi la Watu wa China
kwa gharama ya Shilingi Bilioni 67.87 na kitatumika kutoa mafunzo ya
kijeshi ya kisasa yatakayowawezesha askari kukabiliana na vitisho vya
kisasa vya kiusalama.
Kabla
ya kuzindua kituo hicho Mhe. Rais Magufuli na Balozi wa China hapa
nchini Mhe. Wang Ke wameshuhudia makabidhiano ya kituo hicho kutoka
Jeshi la Ukombozi la Wananchi wa China lililowakilishwa na Naibu Mkuu wa
Idara ya Mafunzo na Utawala ya Kamisheni Kuu ya Jeshi hilo Jenerali
Yang Jian kwenda kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)
lililowakilishwa na Meja Jenerali Yakub Hassan Mohamed.
Mhe.
Rais Magufuli pia ameshuhudia mazoezi ya kijeshi yaliyofanywa katika
kituo hicho yakiwemo shambulizi la kutokea baharini (amphibian landing),
makomandoo kukabiliana na magaidi na kupiga shabaha kwa kutumia
miundombinu ya kisasa.
Akizungumza
na Maafisa, Askari na wananchi waliojitokeza kushuhudia tukio la
makabidhiano ya kituo hicho Mhe. Rais Magufuli amelishukuru Jeshi la
Ukombozi la Watu wa China na Serikali ya China kwa kutoa msaada wa
kujengwa kwa kituo hicho na amesema Serikali ya Awamu ya Tano inathamini
na kutambua mchango wa China katika Jeshi la Ulinzi la wananchi wa
Tanzania.
Mhe.
Rais Magufuli amesema China imeendelea kudhihirisha urafiki na udugu
wake na Tanzania kwani licha ya kujenga kituo hicho pia imetoa msaada wa
kujenga kituo cha mafunzo ya kijeshi ya anga cha Ngerengere Mkoani
Morogoro na miradi mingine ya maendeleo ya jamii na hivyo amemuomba
Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke kufikisha shukrani zake kwa
Rais wa China Mhe. Xi Jinping.
Mhe.
Wang Ke na Jen. Yang Jian wamesema China imejenga kituo hicho cha
mafunzo maalum ya kijeshi ambacho ni alama nyingine ya uhusiano na
ushirikiano wa kirafiki na kidugu kati yake na Tanzania na wameipongeza
JWTZ kwa kupata kituo ambacho wanaamini kitatumika kuimarisha ulinzi na
usalama wa Tanzania na nchi nyingine za Afrika.
Mkuu
wa Majeshi ya Ulinzi nchini Jenerali Venance Salvatory Mabeyo amesema
miundo ya kituo hicho inakifanya kuwa kituo cha kimataifa kilicho bora
zaidi Afrika Mashariki na Kati kitakachoweza kutoa mafunzo ya kisasa kwa
askari wengi na amemuomba Mhe. Rais Magufuli kusaidia ujenzi wa daraja
la mto Mpigi litakalokiunganisha na barabara ya kwenda Dar es Salaam.
Pamoja
na kukubali ombi hilo Mhe. Rais Magufuli pia amekubali maombi ya Jen.
Mabeyo ya kupeleka maji, umeme na barabara katika eneo ambalo China
imekubali kutoa msaada wa kujenga makao makuu ya JWTZ Mkoani Dodoma na
ameahidi kuziagiza wizara husika kutekeleza maombi hayo haraka.
Tukio
la kukabidhiwa kwa kituo cha mafunzo maalum ya kijeshi limehudhuriwa na
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi na
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine
Mahiga.
Wakati huo huo,
Mhe. Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Mapinga waliosimamisha
msafara wake na kumuomba awasaidie kulipwa fidia kufuatia maeneo yao
kuchukuliwa kwa ajili ya miradi ukiwemo mradi wa ujenzi wa kituo hicho
cha mafunzo cha jeshi na kuvunjiwa nyumba zao katika eneo la Makurunge.
Katika
majibu yake Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali haiwezi kurudia
kuwalipa watu ambao tayari walishalipwa fidia na hawezi kuwatetea watu
ambao wamevunja sheria kwa kuvamia maeneo yasiyokuwa yao.
Mhe.
Rais Magufuli pia amesema Serikali ina dhamira ya dhati ya kutekeleza
mradi wa bandari na eneo la uwekezaji la Bagamoyo na amewataka watu wote
waliolipwa fidia wakati hawakuwa na maeneo warejeshe fedha za Serikali,
waliolipwa fidia kuondoka katika maeneo yaliyolipiwa, na kwa wale ambao
hawajalipwa fidia waendelee kutumia maeneo yao kwa shughuli zao
mbalimbali.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Februari, 2018