MWENYEKITI WA UVCCM ALIYEDAKWA KWA RUSHWA AACHIWA HURU MAHAKAMANI
Mahakama ya hakimu mkazi Mkoa wa Dodoma
imemwachia mwenyekiti wa zamani wa Umoja wa Vijana wa Chama cha
Mapinduzi (UVCCM), Sadifa Juma Khamis baada ya upande wa Jamhuri
kuwasilisha maombi ya kuifuta kesi iliyokuwa ikimkabili.
Uamuzi huo umetolewa leo Februari 15,
2018 na hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo, Emmanuel Fovo baada kuridhia
ombi la wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),
Biswalo Biswalo kuiomba mahakama kuifuta kesi hiyo.
Desemba 9, 2017, Sadifa alikamatwa na
Takukuru akiwa nyumbani kwake Mailimbili mjini hapa akituhumiwa kugawa
rushwa kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa umoja huo.
Mbunge huyo wa Donge na mjumbe wa kamati
kuu ya CCM aliyemaliza muda wake, baada ya kukamatwa alilala mahabusu
kwa siku tatu baada ya kukosa dhamana.
Katika shtaka la kwanza, Sadifa alidaiwa
aliwahonga wanachama ili wamchague Rashid Mohamed Rashid ambaye alikuwa
akiwania umakamu mwenyekiti katika uchaguzi mkuu wa umoja huo.
Shtaka la pili, alidaiwa kuwaahidi
kuwalipia gharama za usafiri wanachama wa umoja huo kwa kuwasafirisha
kutoka Dodoma hadi Kagera kama zawadi ili wamchague Rashid.
Na Sharon Sauwa,Mwananchi