MAHAKAMA YAFUNGA JALADA LA KESI YA MOBETO DHIDI YA DIAMOND PLATNUMZ
Jalada la kesi ya madai ya matunzo ya
mtoto, Prince Abdul lililofunguliwa na mwanamitindo Hamisa Mobeto dhidi
ya msanii Nasseb Abdul maarufu Diamond Platnumz limefungwa rasmi katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu upande wa watoto.
Leo Februari 13, 2018 baada ya kutoka
mahakamani hapo, Diamond amesema walifika kwa ajili ya kuweka kumbukumbu
sawa upande wa ustawi wa jamii na mahakama.
Amesema wanategemea mtoto wao kuwa
kiongozi huku akiwashauri wazazi kuweka majivuno pembeni wanapokuwa na
migogoro na wasimuingize mtoto.
"Nalazimika kuweka majivuno pembeni ya
matatizo yetu binafsi kwa kuwa mtoto ndiyo anaumia, ni lazima muangalie
ni namna gani mnatengeneza mazingira mazuri ya kuweza kumlea na
kumsaidia mtoto,” amesema Diamond.
Naye wakili wa Mobeto, Walter Godluck
amesema ustawi wa jamii unasaidia katika usuluhishi wa kesi za watoto
zinazohusu malezi ambapo baba na mama hukubaliana ni jinsi gani wanaweza
kulea mtoto.
“Malalamiko waliyoyaleta kuhusu malezi
ya mtoto upande wa pili wameridhia na wameona kuna haja ya kuyafanyia
kazi. Kiasi cha fedha wamekubaliana ila wamekiweka kifamilia,” amesema
Godluck.
“Wazazi wamekubali kushughulikia malezi
ya mtoto. Diamond yupo tayari kumlea mtoto na yupo tayari kulifanya hilo
kwa kadri inavyowezekana.”
Hamisa Mobeto amesema amefurahia maamuzi hayo kwa kuwa pande zote mbili walikaa na wakakubaliana.
Mobeto alifungua kesi hiyo mahakamani hapo, pamoja na mambo mengine alikuwa anaomba matunzo ya mtoto waliozaa na msanii Diamond.
Aliiomba mahakama imwamuru Diamond kutoa
matunzo ya mtoto huyo kila mwezi. Alifungua kesi hiyo kupitia mawakili
wake Abdullah Lyana na Godluck kutoka kampuni ya uwakili ya Century
Attorneys.
Kupitia hati hiyo ya madai, Mobeto anaomba Diamond amuombe msamaha kwa kumsababishia madhara yaliyoishtua familia yake.
Diamond aliwasilisha hati ya majibu
kinzani akipinga maombi hayo ya Mobeto akidai gharama anazodai kulipwa
kwa mwezi ya Sh 5 milioni kwa ajili ya matunzo ya mtoto ni kubwa hawezi
kuzimudu.
Na Tausi Ally, Mwananchi
