JINSI MWANAFUNZI ALIVYOUAWA KWA KUPIGWA RISASI NA POLISI CHADEMA WAKIANADAMANA DAR
Kamanda
wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amekiri mtu
mmoja kupigwa risasi na polisi, wakati wakiwatawanya wafuasi wa Chama
cha demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), walioandamana jana Februari 16,
2018.
Wafuasi hao wa CHADEMA wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman
Mbowe waliandamana kuelekea ofisi ya msimamizi wa uchaguzi Jimbo la
Kinondoni, Aron Kagurumjuli kudai viapo vya mawakala wa uchaguziwa chama
hicho.
Maandamano hayo yalianzia viwanja vya Buibui Mwananyamala ulikokuwa
ukifanyika mkutano wa kampeni wa Chadema na yalipofika eneo la Mkwajuni
wafuasi hao walitawanywa na polisi, huku mtu mmoja aliyekuwa kwenye basi
la daladala akidaiwa kupigwa risasi na kufariki dunia
Kamanda Mambosasa amesema kuwa watu hao waliokuwa wakiandamana, walizuia
mabasi yanayotoa huduma ya usafiri wa mwendokasi, na kuanza fujo kwa
kurusha mawe, hivyo polisi waliingilia kati na kuwatawanya kwa kufyatua
risasi kadhaa hewani, na kati ya risasi zilizofyatuliwa, moja ilimpata
mtu.
“Walizuia mwendo kasi, wakaanza kupiga mawe kwa hiyo kati ya risasi za
hewani zilizopigwa kuwatawanya kuna iliyompata (mtu),” alisema.
Ufafanuzi huo wa Mambosasa licha ya kutoweka wazi kama mtu huyo
aliyepatwa na risasi hiyo amefariki dunia ama la, umekuja huku ikidaiwa
kuwa aliyepigwa risasi na kupoteza maisha ni mwanafunzi wa elimu ya juu.
Taarifa za kifo cha mwanafunzi huyo zilianza kusambaa tangu jana, Ijumaa
jioni katika mitandao ya kijamii sambamba na kuwekwa picha yake huku
ikieleza kuwa amepigwa risasi wakati akiteremka katika basi la daladala.
Mambosasa alipoulizwa kama mtu huyo ni mwanafunzi wa elimu ya juu
amesema kuwa haijathibitishwa kama ni mwanafunzi na bado uchunguzi
unaendelea ili kubaini ukweli wa jambo hilo.
“Haijathibitishwa hiyo, nipo kwenye pilika za uchaguzi, nadhani nitajibu hilo nitakaporejea ofisini na kupata taarifa,” alisema.