Sugu Amkataa Hakimu Akidai Anapendelea
Mbunge
wa Mbeya Mjini 'Sugu' na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu
Kusini, Emmanuel Masonga wamemkataa Hakimu Mkazi Mfawidhi, Michael
Mteite wakidai hawana imani naye katika mwenendo wa kesi hiyo.
Sugu
na Masonga wanashtakiwa kwa kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya
Rais John Magufuli wanayodaiwa kuitoa Desemba 30,2017.
Washtakiwa
leo Alhamisi Januari 25,2018 asubuhi wamefika katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Mbeya kwa ajili ya kuanza kutoa ushahidi baada ya upande wa
Jamhuri kukamilisha na kufunga ushahidi wao.
Upande wa Jamhuri umewasilisha mashahidi watano mahakamani na vielelezo viwili ikiwamo sauti iliyorekodiwa.
Baada
ya utaratibu wa kimahakama kukamilika ili kuanza ushahidi, wakili
Boniface Mwabukusi anayewawakilisha Sugu na Masonga alimuomba hakimu
Mteite akisema wateja wake wana jambo la kuieleza Mahakama.
Hakimu
alipowaruhusu kuzungumza, Sugu ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika
kesi hiyo, amesema kutoka ndani ya nafsi yake ameitafakari kesi na
mwenendo wake na kufikia uamuzi wa kumkataa hakimu kwa kuwa hana imani
naye kwa sababu tatu.
Amesema,
“Naomba niitaarifu Mahakama hii kwamba nimetafakari mwenendo wa kesi
hii, mimi mshtakiwa wa kwanza Joseph Mbilinyi naona nikukatae wewe
hakimu kutokana na mambo yafuatayo: kwanza; sijawahi kuona hakimu yuko
biased (wenye upendeleo) kama ulivyo wewe, ulivyoninyima dhamana bila
sababu za kisheria na Katiba.”
“Pili,
jana nimeshuhudia kielelezo cha tape recorder kikitokea mikononi mwa
wakili wa serikali ambacho wakili wangu (Mwabukusi) alikikana na
ukamshambulia sana wakili wangu kwamba wakati anakitoa yeye (wakili)
alikuwa ametoka wakati mimi nilikuwa hapa sikuona. Sasa kitendo kile
naona wewe hakimu una interest (masilahi) dhidi yangu,” amesema.
Sugu
amesema, “Lakini pia jana ulikiri kwamba katika kesi hii unapata
mateso, hivyo mimi ni Mkristo, sasa ili nisikupe tabu na mateso naomba
nikukatae na apangiwe hakimu mwingine atakayeendesha kesi hii kwa uhuru
na haki.”
Amesema kwa sababu hizo anaomba amkatae hakimu huyo.
Baada ya ombi hilo la Sugu, hakimu Mteite alimpa nafasi Masonga ambaye pia alimkataa akitoa msimamo unaofanana na wa Sugu.
Katika
sababu zake, Masonga amesema, “Mheshimiwa jana ulipotoa uamuzi wa
kupokea vielelezo kutoka kwa upande wa Jamhuri, wa tape recorder na
register mheshimiwa hakimu ulieleza Mahakama yako kwamba unaruhusiwa
kisheria wakati upande wa Jamhuri ulikubali ushahidi upokewe kama Id
(utambulisho) lakini register ipokewe kama kidhibiti. Lakini bado
uamuzi wako ulikuja tofauti na upande wa Jamhuri.”
Amesema,
“Ulipofanya uamuzi wakati tulipokuomba dhamana, ulisema unakubaliana na
hoja za pande zote mbili (utetezi na Jamhuri). Na Jamhuri walisema kwa
ajili ya usalama wetu (washtakiwa), wanaomba tusipewe dhamana. Na wewe
katika uamuzi wako umezingatia hoja zao lakini umezingatia zetu kwa
sababu ni haki yetu kisheria na kikatiba. Na uamuzi wako ulisema unazuia
dhamana kwa sababu unataka kesi hii iendee haraka, bila kujadili hoja
zilizoletwa mbele yako.”
Hakimu Mteite amesema amezingatia hoja hizo na atatoa uamuzi baada ya saa moja.