DR SLAA : NILIKUWA NAMPENDA RAIS MAGUFULI TANGU NIKIWA MBUNGE UPINZANI
ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa amesema alimpenda
Rais Dk. John Magufuli tangu akiwa Mbunge wa Karatu.
Dk. Slaa ambaye alitangaza kuachana na
siasa mwaka 2015 kwa kutofautiana na chama chake katika kumpokea Waziri
Mkuu wa zamani Edward Lowassa, alitoa kauli hiyo jana alipokutana na
Rais Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam.
Novemba 22 mwaka jana, Rais Dk.Magufuli
alimteua Dk. Slaa kuwa balozi siku chache baada ya gazeti hili kuripoti
taarifa za kiongozi huyo zamani wa Chadema, kuajiriwa katika duka kubwa
la bidhaa za majumbani (Supermarket) la Costco lililopo Oakville,
Toronto nchini Canada.
Dk. Slaa aliongoza jimbo hilo kwa
vipindi vitatu mfululizo kuanzia mwaka 1995 hadi 2010, baada ya
kuteuliwa na Chadema kuwania urais.
Katika mazungumzo hayo pamoja na mambo
mengine Dk. Slaa alisema huwa wapinzani wanawekwa pembeni lakini yeye
hakuwahi kuwekwa kando na Rais Magufuli wakati huo akiwa waziri.
“Ni kweli kukupenda (Rais Magufuli)
haikuanza leo ni tangu ukiwa waziri tukiwa bungeni ulifika Karatu
hukuniweka pembeni nadhani si kawaida kwa sababu wapinzani huwa
wanawekwa pembeni mara nyingi lakini mimi hukuniweka pembeni,” alisema
Dk. Slaa.
Alisema akiwa upinzani alipiga kelele
kwa sababu kulikuwa na upungufu lakini kwa sasa ana furaha kwani yale
ambayo alikuwa akiyapigia kelele yametekelezwa.
“Wakati ule nilipiga kelele kwa sababu
nilikuwa naona kwamba kuna upungufu, leo nina furahi yale ambayo
nilikuwa nayapigia kelele yanatekelezwa kwa sababu nimeyaona…sasa kitu
kikubwa ni macho.
“Ushabiki katika maendeleo hauna tija,
ushabiki katika siasa nao hauna tija. Kama nilivyoeleza huko nyuma siasa
ni sayansi wapo wanaofikiri kuwa siasa ni upotoshaji.
“Sasa siasa kama ni sayansi ina misingi
yake ambayo inahitaji kusimamiwa, utendaji wa Rais una mambo kadhaa ya
msingi ambapo jambo la kwanza; ni mtu mwenye maono au hapana, nafiriki
Rais ana mtazamo kwa sababu huwezi kubuni mengi ya mambo haya
yaliyofanyika kwa muda mfupi kama huna mtazamo.
“La pili ni uthubutu; si watu wengi sana
wanaweza kufikiria kufanya jambo na ndani ya muda mfupi, akaweza
kutafuta njia ya kukitekeleza jambo hilo, unapokuwa jasiri unachukua
hatua kwa sababu unaamini unachofanya ni kwa ajili ya manufaa ya nchi
yako,”alisema Dk. Slaa.
Kwa upande wake, Rais Dk. Magufuli
alimpongeza Dk. Slaa kwa moyo wake wa kizalendo huku akisema alimteua
kuwa balozi kwa kuwa anatambua ataweza kupigania masilahi ya Tanzania
popote atakapopangiwa kuiwakilisha.
“Dk. Slaa alinijulisha kuwa anakuja na
akaomba akija angependa kuja kuniona na nikampangia leo (jana),
tumezungumza mambo mengi na ameniahidi kuwa atakwenda kufanya kazi yake
vizuri kwenye nchi atakayokwenda kuwa Balozi.
“Dk. Slaa ni mtu safi, anazungumza
kutoka moyoni na anaipenda Tanzania na mimi kutokana na moyo wake wa
kuchukia ufisadi na kuchukia wizi nikaamua kumteua kuwa Balozi,” alisema
Rais Dk. Magufuli.
Uamuzi wa Dk. Magufuli kumsifu Dk. Slaa
kwa mara ya kwanza alimsifu kiongozi huyo wakati wa kampeni za Uchaguz
Mkuu wa mwaka 2015, alipokuwa akiomba kura wilayani Karatu ambapo
alimsifu kutokana na msimamo wake wa kizalendo ikiwemo kukataa
kukumbatia ufisadi.
Alisema kama Dk. Slaa, angekuwa anagombea ubunge angemnadi bila kujali chama chake anachotoka.
Wakati huohuo, Rais Magufuli aliagana
jana na maofisa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambao
wamestaafu baada ya kutimiza umri.
Walioagana na Rais ni Luteni Jenerali
James Mwakibolwa aliyekuwa Mnadhimu Mkuu wa (JWTZ) na Meja Jenerali
Michael Isamuhyo aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Wengine ni Brigedia Jenerali Aron
Lukyaa, Brigedia Jenerali William Kivuyo, Brigedia Jenerali Elizaphani
Marembo na Kanali Peter Samegi.
CHANZO - MTANZANIA