Mabasi yakamatwa usiku wa manane kwa mwendokasi
Mabasi
saba ya abiria yamekamatwa na kutozwa faini kwa kosa la mwendokasi na
kutofuata sheria za usalama barabarani huku wakihatarisha maisha ya
abiria.
Kamatakamata
hiyo ambayo imesimamiwa na Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani
Fotunatus Muslim akiwa na timu ya viongozi na askari mkoa wa Morogoro
imefanyika usiku wa kuamkia leo.
Zoezi
la ukamataji mabasi hayo limefanyika eneo la Dumila Wilaya ya Kilosa
mkoani hapa, zoezi lilichukua takribani masaa mawili ambapo mabasi hayo
yamezuiwa kuondoka mpaka asubuhi huku yakitozwa faini.
Kamanda Muslim amesema jeshi hilo halitakubali kuona maisha ya watanzania yakipotea kutokana na uzembe wa baadhi ya madereva.
Amesema
kikosi hicho cha usalama barabarani kimeahidi kupambana na madereva wa
mabasi ya abiria hasa nyakati za usiku kwani ndio wamekuwa wakiendesha
kwa mwendokasi huku wakidai serikali muda huo inakuwa imelala.
Mabasi
ya abiria zaidi ya saba yanayofanya safari kati ya mkoa wa Mara
(Musoma) Dar es salaam, na Mwanza- Dar es salaam yamekaguliwa na kutozwa
faini.
Muslim
amesema madereva wengi wamekuwa wakifuata sheria za barabarani nyakati
za mchana kwa kuhofia kukamatwa kutokana na tochi zilizopo na inapofika
nyakati za usiku madereva hao wamekuwa wakitumia mwanya wa kuendesha
kwa mwendo kasi.
Akizungumzia
dhamira ya Polisi Muslim amesema ni kuwalinda raia na mali zao na
kuwataka askari wa usalama barabarani kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Amesema
doria ni endelevu na sasa itakuwa kwa nchi nzima kwa usiku na mchana
huku akiwataka madereva hao kuacha kudanganyika kwa madai kuwa tochi
usiku hazifanyi kazi usiku na kwamba tochi sasa zitakamata mpaka usiku.
"Nimekuja
na slogani ya Kamata hii ni kwa wale madereva wasiotii na kufuata
sheria na tutapambana nao kila wakati na nyakati zote na hiyo itasaidia
abiria kusafiri salama na matumizi ya barabarani kuwa bora," amesema
kamanda Muslim
Mmoja
wa abiria aliyejitambulisha kwa jina la Leon Mwete aliyekuwa katika
moja ya basi yaliyokamatwa eneo hilo la Dumila amesema zoezi hilo ni
zuri na linafaa kuendelea.
Amesema hii itapunguza ajali za barabarani na kwamba kwa sasa uendeshaji wa madereva wengi ni mzuri ukilinganisha na zamani.
Naye
kamanda wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Morogoro Boniface Mbao
ameeleza kuwa yeye akiwa msimamizi mkuu ataendelea kusimamia na kufanya
oparesheni za usiku na mchana kama maelekezo yaliyotolewa.