Kimenuka Tena......Ripoti ya Madini ya Tanzanite Yaibua UOZO Mzito Ukiwahusisha Mawaziri wa Sasa na Wa Zamani
Uko
uwezekano mkubwa wa Baraza la Mawaziri kutikisika baada ya mawaziri
kadhaa waliopo na wale walioondolewa kutajwa mara kadhaa katika taarifa
za kamati maalumu za bunge kuchunguza biashara ya Tanzanite na almasi.
Aidha
taarifa zote mbili ziliwataja kwa majina watu kadhaa wakiwemo mawaziri
waliopo katika baraza la sasa kwa kujihusisha moja kwa moja katika
maamuzi yaliyopindisha sheria na kukiuka utaratibu.
Kamati
zote mbili zilizungumzia kwa undani hasara kubwa zilizopatikana
kutokana na ushauri mbovu na usimamizi dhaifu katika mkataba wa kuuza
hisa katika kampuni ya almasi mwaka 1994 ambao hazikusaidiwa na pia ubia
wa Stamico na Tanzanite One Mining Limited (TML) ambapo unaelezwa
uliharakishwa na Waziri George Simbachawene.
Pia,
Stamico ilionekana kutofuatilia mikataba yote huku baadhi ya watendaji
wa sasa wakibariki ubia huo na kusema kwamba ulikuwa ni msaada mkubwa
kwa Stamico.
Pia
imeelezwa kuwa hakuna taarifa sahihi kuhusu uzalishaji na uuzaji wa
tanzanite ingawa duniani mauzo ni dola trilioni 8.582 katika miaka 12
iliyopita huku takwimu za Tanzania zikionesha kwamba mauzo ni bilioni
454 tu kwa kipindi hicho.
Imeelezwa kuwa ni asilimia 20 ya uuzaji wa tanzanite unajulikana nchini lakini 80 husafirishwa kwa njia ya panya.
Aidha,
katika uchunguzi uliofanywa na kamati hizo ulibaini kwamba baraka
zilizotolewa kwa Sky zilikuwa kinyume kwani kampuni hiyo haina usajili
nchini wala haitambuliki brela.
Waziri mkuu anena
Taarifa
za kamati maalumu za Bunge zilikabidhiwa jana kwa Spika wa Bunge kabla
ya yeye naye kukabidhi kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye naye
alisema kwamba anazifikisha kwa Rais John Magufuli leo saa nne na nusu
kwa hatua zaidi.
Akizungumza
baada ya kupokea taarifa hizo Waziri Mkuu alishukuru kazi njema
iliyofanywa na kamati hizo na kuahidi kwamba yote yaliyozungumzwa
yatafanyiwa kazi katika kipindi kifupi kijacho.
Alisisitiza
kuwa serikali ya awamu ya tano kamwe haitamwacha mtu ambaye anakiuka
katiba kwa kuacha kulinda maliasili za taifa huku akikariri Ibara ya 27
ya katiba ya mwaka 1977 kama muhuri tosha kwa kila Mtanzania.
“27
(1) kila mtu ana wajibu wa kulinda mali asilia ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania mali ya Mamlaka ya Nchi na mali yote inayomilikiwa kwa
pamoja na Wananchi na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine.
“(2)
Watu wote watatakiwa na Sheria kutunza vizuri mali ya Mamlaka ya nchi
na pamoja vita aina zote za uharibifu na ubadhilifu na kuendesha uchumi
wa Taifa na kuendesha uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndiyo
waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa lao.” Alisema serikali itaendelea na
jitihada za kuleta mageuzi katika madini ili rasilimali hizo zinufaishe
Watanzania wote.
Pamoja
na hatua za haraka kuchukuliwa alisema kwamba sheria ya madini, petrol,
kodi ya mapato zitafanyiwa marekebisho ili kuimarisha mifumo ya
kusimamia madini na rasilimali nyingine za taifa.
Alisema
ni lazima kuchukua hatua kali kwa wahusika wote na kuwataka Watanzania
kwenda pamoja katika vita hiyo iliyoanzishwa na Rais John Magufuli.
Mmoja
wa mawaziri aliyetajwa mara kadhaa kwa ni George Simbachawene ambaye
kwa sasa ndiye Waziri katika Ofisi ya Rais Tamisemi ambaye alishawahi
kuwa Waziri wa Nishati na Madini.
Waziri
huyo alitajwa kuhusiana na biashara ya Tanzanite ambaye aliridhia
mabadiliko katika mauzo ya kampuni uchimbaji Tanzanite na utoaji wa
leseni kinyume na utaratibu.
Aidha
Naibu Waziri Edwin Ngonyani naye ametajwa hasa kuhusiana na kadhia ya
kuzuia serikali kununua mgodi wa almasi kwa dola milioni 10 na
kuikosesha serikali zaidi ya dola milioni 300, fedha ambazo zilienda kwa
kampuni iliyonunua hisa.
Aidha
kamati hiyo ilihoji namna ambavyo walioshiriki kukataa serikali kununua
mgodi huo wa almasi walivyopata bahati ya kuchaguliwa katika bodi ya
waliouziwa hisa.
Aidha
taarifa zote mbili zimehoji tabia iliyooneshwa na watendaji mbalimbali
wa kutochukua maamuzi na kuishia kusema kwenye mahojiano kwamba waliona
ni upuuzi na wizi mtupu kuendelea kufuatia masuala ya ndani yanayogusa
mikataba na uendeshaji.
Kitendo
cha Eliakim Maswi kusema kwamba alipatwa na hasira baada ya kutoka
katika mgodi huo wa almasi na kujionea madudu na kuapa kutokanyaga tena
kulielezwa na kamati hizo kuwa moja ya sababu ya watendaji kuacha mambo
yakiharibika.
Aidha
aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo alitajwa
kupindisha mambo kadhaa na kufanya maamuzi bila kushirikisha bodi
zinazotakiwa na hivyo kusababisha hasara kubwa.
Watu
wengine waliotajwa katika taarifa zote mbili ni pamoja na aliyekuwa
Katibu Mkuu Nishati na Madini, Eliakim Maswi, aliyewahi kuwa Waziri wa
Nishati na Madini, William Ngereja, mwanasheria wa zamani George Werema
Pamoja
na kuelezwa kuwa serikali imepata hasara ya matrilioni kutokana na
mikataba mibovu, na kukosekana kwa uaminifu miongoni mwa watendaji na
watumishi wa umma, pia kuna makampuni yanachimba almasi na kuuza bila
kufuata utaratibu. Makampuni yaliyotajwa ni matatu yakiwemo Caspian na
Midwest.
Mikataba
iliyozungumzwa na kuambiwa ina walakini mkubwa ni pamoja na umiliki wa
Mwadui na mkataba wa Stamico na Tanzanite One Mining Limited, mkataba
ambao ulizaa migogoro ya madeni makubwa kwa upande wa Stamico na kuiacha
ikiwa hoi na deni la dola milioni 4. Spika Job Ndugai alisema
kutojipanga kwa watu wa Stamico kumefanya kampuni hiyo kuingia katika
hasara kubwa huku sera zikiwa hazifuatwi wala sheria.
Ukiukaji
wa kitaasisi Kuwepo kwa ukiukaji wa taratibu na kanuni za kitaasisi na
kiutendaji pia zilielezwa kutoa mwanya wa kampuni ndani ya mgodi wa
almasi wa Mwadui kufanya wanachotaka, huku takwimu za uzalishaji na
mauzo za TMA na Wizara ya Nishati na madini zikipishana.
Aidha
hata akiba ya almasi iliyopo imeelezwa kuwa si ya uhakika kutokana na
serikali kutojua akiba hiyo ikitegemea taarifa zaidi kutoka kampuni ya
Mwadui ambayo kwa muda sasa wanasema wametengeneza hasara na hivyo
kutolipa kodi Kampuni ya Mwadui imekuwa hailipi kodi kuanzia mwaka 2007
hadi 2017 kwa kisingizio kwamba wamepata hasara, hali ambayo haiendi
sambamba na uwekezaji mkubwa unaoendelea hadi mwaka 2023.
Kamati
ilisema usahihi wa takwimu ndiyo msingi wa kufanya biashara, lakini
wakati Williams wanazo takwimu na wanazitumia taasisi za serikali na
serikali yenyewe takwimu zake zinagongana huku nyingine zikionekana
‘kupikwa’ kutokana na kuwiana wakati sheria na muda ni tofauti.
Aidha
takwimu hizo zimekuwa haziendi kwenye uhalisia wa kipindi cha sheria na
maagizo ya kisheria yaliyopo. Tofauti kubwa inayooneshwa katika takwimu
za wizara na taasisi ya TMAA za uzalishaji na pia na TRA katika mauzo.
Katika
maelezo yote kamati ya Zungu ilihoji fedha kiasi cha Sh bilioni 7 na
milioni 700 ambazo hazijaingia serikalini wakati inajulikana pia kwamba
almasi ya Tanzania ndiyo ghali lakini inauzwa kwa bei ya kutupwa katika
soko.
Aidha
kumezuka sintofahamu ya akaunti ya mrabaha kutoka kampuni ya almasi
ambapo inadaiwa ilifunguliwa akaunti NMB ambayo hata katibu mkuu alikuwa
haifahamu, huku suluhu ya kibenki ikiwa haitumiki kuoanisha takwimu za
mapato.
“Mrabaha
wa bilioni 100 ulivyopokelewa na kuhamishwa katika kaunti haueleweki,”
inasema taarifa hiyo ikionesha kuwapo na ubadhirifu mkubwa wa fedha
kutokana na kukosekana kwa uwajibikaji na ufuatiliaji.
Pamoja
na mikataba mibovu kuna shida ya uangalizi wa almasi yenyewe ambapo
hata watendaji wa serikali (walinzi) hawapo katika maeneo nyeti kama
katika x ray na chumba maalumu cha hifadhi; huku Williamson wakiuweka
mgodi wa almasi rehani kufuatia madeni ambayo kiukweli hayajapitishwa
wala kuhakikiwa na Benki Kuu kwa mujibu wa sheria.
Kwa
mujibu wa taarifa za takwimu Tanzania kwa namna ilivyo sasa imeweka
rehani almasi yenye thamani ya trilioni 80 na milioni 800. Ilielezwa
kuwa kuna deni la dola milioni 238 ambalo halijahakikiwa na benki kuu
wala halijulikani limefikia hapo kwa namna gani ni muhimu kuangaliwa.
Ushauri
wa kamati Kwa upande wa kamati ya Dk Bitego iliyochunguza tanzanite
kuna haja ya kuwawajibisha wote waliohusika kuliingiza taifa hili katika
mikataba mibovu isiyokuwa na tija na kuleta hasara.
Aidha
wametaka watumishi waliotajwa wote kuhojiwa tumefikaje hapa huku
wakitaka kutungwa sheria maalumu kuhusiana na madini hayo yanayopatikana
Mererani pekee duniani kote.
Wakati
huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli
anapokea taarifa hiyo ya uchunguzi wa madini kutoka kwa Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, Ikulu Dar es Salaam
leo.