CHADEMA Yapingana na Jeshi la Polisi

Baraza la vijana CHADEMA (BAVICHA) limepinga kauli alizotoa Kamishna Kanda maalumu ya Dar es salaam, Lazaro Mambosasa kuhusu maombi yao kitaifa kumuombea Mbunge Tundu Lissu na kusema wao hawajapanga kuandamana bali watafanya maombi kumuombe Lissu.

Akiongea jana  na waandishi wa habari Katibu Mkuu (BAVICHA) Taifa, Julius Mwita alisema kuwa wameshangazwa na kusikitishwa na kauli kadhaa alizozitoa Mambosasa kuhusu maombi yao na kusema ametafsiri ndivyo sivyo kauli zao kwani wao hawajapanga kufanya maandamano.

"Tumeshangazwa na kusikitishwa na kauli kadhaa alizozitoa Mambosasa akionesha kuwa amezuia maombi hayo kwa sababu alizodai kuwa yatakuwa ni maandamano na kinyume cha taratibu. Tungependa kusema shughuli yetu ya Jumapili haijapangwa kuhusisha wala haitahusisha maandamano yoyote kama ambavyo SACP Mambosasa ametafsiri. "

Julius Mwita aliendelea kuweka wazi kwamba wameamua kukutana kwenye uwanja huo ili kutoa nafasi kwa watu wa imani zote kuweza kukutana na kufanya sala na dua kwa pamoja.

"Tumesema wazi katika taarifa yetu kwa jeshi hilo wilayani Kinondoni, kuwa shughuli ambayo tumeiandaa inahusu maombi ambayo yatahusisha watu wa imani za dini mbalimbali ambao kimsingi hawawezi kukutana ndani ya nyumba moja ya ibada lakini wote hao wanaweza kukutana sehemu moja, mahali pa wazi na kuomba dua/ sala kwa utulivu pamoja" alisema Julius Mwita

Mwita amesema wao wanaendelea na maandalizi ya shughuli hiyo kama kawaida kwa kuwa waanamini hakuna utaratibu wala sheria ambayo wamevunja na kumtaka Mambosasa aipokee hiyo barua ya maombi yao kisha aitafakari na kulinganisha na kauli zake alizozitoa leo mbele ya waandishi wa habari.

"Tunaelewa sheria na taratibu za nchi zinazosimamia mikusanyiko mbalimbali haziwapatii Polisi mamlaka yoyote ya kuzuia mikusanyiko au kutoa kibali cha mikusanyiko, bali sheria na taratibu hizo zimeelekeza wahusika wa shughuli hiyo kutoa taarifa Polisi na kueleza siku, mahali, muda na wahusika wa mkusanyiko husika." 

Mwita aliendelea kutoa ufafanuzi juu ya jambo hilo na kudai

"Baada ya kusikia kauli ya SACP Mambosasa, tunatoa wito kama ifuatavyo tunamsihi SACP Mambosasa apate nakala ya barua yetu ya taarifa kuhusu shughuli hiyo ambayo tumepeleka mamlaka za kipolisi kama sheria inavyoelekeza, ili aweze kutafakari uzito wa shughuli hiyo ya maombi ya Kitaifa ya Vijana kisha alinganishe na kauli zake alizotoa leo" alisema Mwita

Mbali na hilo Katibu Mkuu wa (BAVICHA) Julius Mwita alisema wao wanaendelea na maandalizi na kuwataka watu wenye mapenzi mema na taifa na ambao wameguswa na tukio la kinyama na kikatili la kupigwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu kuhakikisha wanafika Jumapili Sinza Darajani katika uwanja wa TP kwa ajili ya maombezi hayo na kusema jambo hilo si la kisiasa kama ambavyo Mambosasa amekuwa akisema.
Powered by Blogger.