BARAZA LA BIASHARA SHINYANGA LABARIKI JUKWAA LA UWEKEZAJI
BARAZA la Biashara
Mkoa wa Shinyanga limeazimia kufanya Jukwaa la Uwekezaji wa Biashara
mwishoni mwa mwezi huu kwa lengo la kutangaza fursa za kibiashara na
uwekezaji uliopo ndani ya mkoa kwa kushirikiana na Kampuni ya Magazeti
ya Serikali (TSN).
Makubaliano hayo yalifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita katika kikao
cha baraza hilo kilichowakutanisha wajumbe 40 kutoka sekta za umma na
binafsi, ambacho mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa mkoa, Zainab Telack
aliyewataka wajumbe wajitokeze ili kutangaza fursa zilizopo ndani ya
mkoa kwa shughuli wanazozifanya.
Ofisa Mipango wa Mkoa, George Andrew aliwasilisha kwa wajumbe wa baraza
hilo taarifa ya lengo la Kampuni ya TSN kuwa wako tayari kusimamia
shughuli hizo za kutangaza fursa za mkoa, kinachotakiwa ni halmashauri
na wadau mbalimbali kutumia jukwaa hilo kuutangaza mkoa ili jamii na
wawekezaji waelewe fursa zilizopo.
“Baadhi ya halmashauri zimekwisha wasilisha taarifa zao kuhusu fursa
walizonazo na kamati tendaji ya baraza la mkoa tayari tumekwisha
kutembelea maeneo ya uwekezaji hayo na mrejesho tumekiwsha peleka kwenye
Kampuni ya TSN kilichobaki ni sisi wenyewe kujipanga ili kuweza
kufanikisha zoezi zima la jukwaa hilo,” alieleza Andrew.
Mkuu wa Mkoa, Telack alisema jukwaa hilo kuletwa mkoani Shinyanga ni
fursa itakayoweza kuutangaza mkoa mambo yake yenye mafanikio ambayo
baadhi ya watu hawayafahamu, lakini yapo hivyo wajumbe wa baraza
walioshiriki wahakikishe wanahamasisha watu kwenye shughuli za kuona
fursa na msimu wa kilimo.
“Tunafahamu azma ya serikali yetu ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais
John Magufuli kuwa tujenge uchumi wa kati na viwanda kwani mafanikio ya
kuwa na uchumi wa viwanda utawezeshwa na wananchi wenye kipato cha kati
ambao wataondokana na matatizo ya ujinga, umaskini na maradhi,” alieleza
Telack.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA)
Mkoa wa Shinyanga, Meshack Kulwa alisema jukwaa hilo litakuwa ni fursa
mojawapo ya kukutana pamoja baina ya serikali, wawekezaji na wakulima,
kueleza changamoto zilizopo ili kuzitatua kwa nia ya kuleta maendeleo
hivyo jitihada zifanyike kufanikiwa.
Wajumbe wa kikao; Dk Ellyson Maeja na Katibu wa Chama cha Wachimbaji
Wadogo Mkoa wa Shinyanga, Gregory Kibusi, walieleza kuwa jukwaa hilo
chini ya uratibu wa TSN kwa kushirikiana na Mkoa na TCCIA, wamelipokea
na watahakikisha fursa za mkoa kwa wafanyabiashara.
IMEANDIKWA NA KARENY MASASY, SHINYANGA