Waziri Mkuu Ampa Siku 15 Mweka Hazina Sikonge........Ataka apate maelezo kwa nini ameshindwa kukusanya mapato
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amempa siku 15 Mweka Hazina wa Wilaya ya Sikonge,
Bw. Evans Shemdoe ajieleze ni kwa nini ameshindwa kufikisha asilimia 80
ya makusanyo ya ndani.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo leo asubuhi (Alhamisi, Agosti 10, 2017) wakati
akizungumza na watumishi na watendaji wa wilaya hiyo, mjini Sikonge.
“Nataka
maelezo yakayoniridhisha ni kwa nini hamkufikisha asilimia 80 ya
makusanyo ya halmashauri ambacho ni kiwango cha chini. Nzega TC
wamefikisha asilimia 112, Kaliua wana asilimia 91, Nzega DC wana
asilimia 80, ni kwa nini wewe umeshindwa kufikisha kiwango hicho?,”
alihoji Waziri Mkuu.
“Ninataka
nipate maelezo pia ni ipi mipango yenu ya kukusanya mapato kwa maeneo
mliyoshindwa kufanya vizuri, na pia mmejipangaje kwa mwaka ujao wa
fedha. Niyapate maelezo hayo ifikapo tarehe 25 Agosti,” amesema.
Alipopewa
nafasi ya kujieleza, Bw. Shemdoe alisema wamefikisha asilimia 76.7 na
wameshindwa kufikia lengo kwa sababu ya upungufu wa mvua katika msimu
uliopita, hali ambayo ilichangia kushuka kwa mavuno ya zao la tumbaku
miongoni mwa wakulima.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu aliwataka watumishi wa wilaya hiyo, washirikiane na
watendaji na madiwani ili kuongeza mapato ya wilaya hiyo badala ya
kuwaachia watendaji wa kata peke yao.
Jana,
mara baada ya kupokea taarifa ya mkoa wa Tabora, Waziri Mkuu alizitaka
Halmashauri tano kati ya nane za mkoa huo zitoe maelezo ni kwa nini
zimeshindwa kufikisha asilimia 80 ya makusanyo kama ambavyo waliagizwa
na Serikali.
“Halmashauri
zilizovuka malengo ni tatu tu, Nzega TC, Kaliua na Nzega DC. Nataka
taarifa za halmashauri zilizobakia ifikapo Agosti 25, wakijieleza ni kwa
nini hawajafikia malengo ya ukusanyaji mapato yaliyowekwa ambayo ni
asilimia 80,” alisema.
Taarifa
ya mkoa huo inaonyesha makusanyo kwa kila Halmashauri ni kama
ifuatavyo:- Tabora Manispaa asilimia 64.1; Nzega Mji (asilimia 112);
Nzega Wilaya (asilimia 80.8); Igunga (asilimia 64.6); Tabora (asilimia
77.3); Sikonge (asilimia 76.7); Urambo (asilimia 70.9) na Kaliua
(asilimia 91.5).
Pia
amezitaka Halmashauri zote zihakikishe zinafanyamakusanyo kwa kutumia
mfumo wa kielektroniki. “Ukusanyaji wote wa mapato ni lazima ufanyike
kwa mfumo wa kielektroniki. Halmashauri ambazo hazijafanya hivyo,
zitumie makusanyo ya mwaka jana kununulia mashine za EFD. Hatutaki kuona
risiti za kuandika kwa mkono zinatumika,” alisisitiza.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu ameutaka uongozi wa mkoa wa Tabora
uhakikishe wanapatikana watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
katika wilaya hiyo ili waweze kusaidiana na watendaji wa halmashauri
hiyo kukusanya mapato.
“Hapa
Sikonge naambiwa hakuna ofisi za TRA. Lazima tupate maafisa wa TRA
katika kila Halmashauri ili watoe elimu na washirikiane na madiwani,
watendaji wa vijiji na watumishi wa Halmashauri juu ya ukusanyaji
mapato,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, AGOSTI 10, 2017.