Serikali Kununua Rada 4 za Kisasa
Mamlaka
ya Udhibiti wa Usafiri wa Anga (TCAA) jana (Jumanne) imeingia
makubaliano na kampuni inayojihusisha na mifumo ya anga kutoka nchini
Ufaransa ya Thales kununua rada mpya nne.
Tukio
hilo lilishuhudiwa na Waziri wa Ujenzi uchukuzi na mawasiliano Profesa
Makame Mbarawa na wadau wengine wa usafiri wa anga nchini.
Upande
wa Serikali mkataba ulisainiwa na Mkurugenzi wa Mkuu wa TCAA Hamza
Johari na upande wa Thales alikuwa ni Meneja wa masoko wa kanda kutoka
kampuni ya Thales Abel Aberr Carr.
Mkurugenzi
wa Mkuu wa TCAA Hamza Johari anasema kwa sasa Tanzania ina rada moja
pekee na uwezo wake kiufanisi umepungua kutokana na mabadiliko
yanayotokea kwa haraka katika sekta hiyo, sanjari na kuongezeka kwa
ndege zinazotumia anga la nchi.
“Mradi
wa rada hizo ni miongoni mwa mipango mikakati iliyopewa kipaumbele cha
juu na menejimenti ya TCAA kwa lengo la kuboresha huduma za uongozaji wa
ndege kwa haraka, tija na kuongeza usalama katika sekta ya usafirishaji
wa anga nchini na duniani,” amesema Johari.
Kwa
upande wake Profesa Mbarawa amesema kufungwa kwa rada hizo kutaongeza
imani ya wadau wa sekta ya usafiri wa anga dunia kuwa na imani na
kutumia anga la Tanzania, hivyo watalii wataongezeka kwakuwa wanajua
usafiri wa anga nchini kwetu ni wa usalama.
“Kupatikana
kwa rada hizo mpya tutaweza kutoa huduma kwa ndege nyingi zaidi na
kulitawala anga letu zima. Ndege zikiongezeka na watalii wakaongezeka
uchumi wetu utapiga hatua” alisema Profesa Mbarawa.
Aidha
kabla ya tukio hilo Waziri Mbarawa alitembelea chuo cha usafiri wa anga
(CATC) ambapo alikutana na changamoto ya ufinyu wa eneo la chuo, ufinyu
wa bajeti ya kununulia vifaa vya mafunzo na upungufu wa wataalamu.