ODINGA : MITAMBO YA TUME YA UCHAGUZI IEBC ILIDUKULIWA...MATOKEO YANA ULAGHAI WA HALI YA JUU
Mgombea urais wa muungano wa upinzani Nasa Raila Odinga amewaambia
wanahabari kwamba wamepata habari kwamba mitambo ya Tume ya Uchaguzi
IEBC ilidukuliwa na matokeo halisi kufanyiwa ukarabati.
IEBC imekuwa ikitangaza matokeo ya awali ya urais mtandaoni, na kwa sasa
matokeo hayo yalikuwa yanamuonyesha Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha
Jubilee akiwa mbele na kura 7,795,083 (54.38%) naye Bw Odinga akiwa na
kura 6,433,161 (44.76%).
Matokeo hayo ni ya kutoka vituo
38561 kati ya vituo 40883 nchini humo.
Kura zilizoharibika kufikia sasa ni 382,705
Bw Odinga, akiandamana na mgombea mwenza wake Kalonzo Musyoka, na
viongozi wengine wakuu wa muungano huo, amesema wadukuzi walitumia
taarifa alizokuwa nazo meneja wa teknolojia wa IEBC Chris Msando
aliyeuawa wiki moja iliyopita kuingia katika mitambo ya IEBC.
Waziri huyo mkuu wa zamani amesema baada ya kuingia, wadukuzi walitumia
programu fulani kuongeza matokeo ya Rais Kenyatta na kupunguza matokeo
yake.
Amesema anaamini hilo lilifanyika katika kaunti zote na kwamba wagombea wa NASA katika nyadhifa nyingine waliathirika pia.
Bw Odinga, amesema huo ulikuwa "ulaghai wa hali ya juu".
Hata hivyo, ametoa wito kwa wafuasi wa muungano huo waendelee kuwa watulivu.
Bw Musyoka amesema anawashauri wafuasi wa muungano huo waendelee na
shughuli zao za kawaida, ingawa huenda karibuni wakatakiwa kuchukua
hatua.
Bw Odinga na Kalonzo wamekataa kusema ni hatua gani zaidi watachukua na
badala yake wakasema wanasubiri kusikia ufafanuzi kutoka kwa IEBC kuhusu
yaliyotokea.
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati amewaambia wanahabari baadaye kwamba
wamepata habari kuhusu tuhuma za muungano huo wa upinzani kwamba
mitambo yao ya uchaguzi ilidukuliwa.
Amesema tume haiwezi kupuuza tuhuma kama hizo na kwamba maafisa wake
watafanya uchunguzi kubaini iwapo kuna ukweli wowote katika madai hayo.
Hata hivyo alieleza imani yake kwamba mfumo wa uchaguzi unaotumiwa na
tume hiyo ni imara na kwamba ulitumiwa na shughuli zote za awali, na
sasa "imesalia shughuli ya mwisho" ya kupeperusha na kutangaza matokeo
ya kura.