Bill Gates amwaga mabilioni Tanzania
Taasisi
ya Bill and Mellinda Gates imetenga Dola za Marekani Milioni 350 sawa
na takribani Shilingi Bilioni 777.084 za Tanzania kwa ajili ya
kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta ya kilimo, afya na mifumo ya
kielektroniki ya upatikanaji wa taarifa.
Mwenyekiti Mwenza wa taasisi hiyo Bw. Bill Gates amesema hayo leo tarehe 10 Agosti, 2017 Ikulu Jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Bw.
Bill Gates amesema kama ambavyo taasisi yake imeshirikiana na Tanzania
kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha huduma za afya hapa nchini, fedha
hizo zitaelekezwa katika utekelezaji wa miradi zaidi ya afya ikiwemo
kupunguza vifo vya uzazi, kukabiliana na ugonjwa wa malaria, kuimarisha
lishe na kukabiliana na utapiamlo, zitaelekezwa katika sekta ya kilimo
ambako zitasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao, kuzalisha mbegu bora na
kuboresha ufugaji utakaoongeza chakula na pia zitasaidia kuweka mifumo
ya kisasa ya upatikanaji wa taarifa.
Bw.
Bill Gates ameelezea kufurahishwa na maendeleo ya uchumi wa Tanzania
pamoja na uongozi na msimamo wa Rais Magufuli juu ya kutaka miradi hiyo
ilete matokeo yenye manufaa, na amesema atakuja Tanzania mara nyingi ili
kuimarisha zaidi ushirikiano na kufuatilia utekelezaji wa miradi.
Kwa
upande wake Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Bw. Bill Gates kwa mchango
mkubwa unaotolewa na taasisi ya Bill and Mellinda Gates katika miradi
mbalimbali hapa nchini ikiwemo fedha ambazo taasisi hiyo itazitoa katika
kipindi cha miaka mitano kuanzia sasa na amemhakikishia kuwa Serikali
yake itahakikisha fedha hizo zinaleta matokeo yaliyokusudiwa.
Mazungumzo
kati ya Mhe. Rais Magufuli na Bw. Bill Gates yamehudhuriwa na Waziri wa
Kilimo, Ufugaji na uvuvi Dkt. Charles Tizeba na Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu.
Wakati
huo huo, Mhe. Magufuli amekutana na kufanya Mazungumzo na Kaimu Balozi
wa Marekani hapa nchini Mhe. Dkt. Inmi Patterson ambaye amesema Marekani
itatoa fedha za nyongeza kiasi cha Dola Milioni 225 sawa na Shilingi
Bilioni 499.500 za Tanzania katika mwaka ujao kwa ajili ya kutekeleza
miradi mbalimbali ya maendeleo itakayogusa sekta za elimu, afya, lishe
bora, utawala bora.
Mhe.
Inmi Patterson amesema Marekani imeongeza fedha hizo katika miradi
inayotekelezwa hapa nchini kwa sababu ina dhamira ya dhati ya
kushirikiana na Tanzania na itahakikisha uhusiano na ushirikiano huu
unaendelezwa na kukuzwa zaidi.
Kwa
upande wake Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Balozi Inmi Patterson
kwa mchango mkubwa ambao Marekani imekuwa ikiutoa kwa Tanzania na
amemhakiki kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza na kukuza zaidi
ushirikiano wake na Marekani, na pia amemuomba awahimize wafanyabiashara
na wawekezaji wengi zaidi wa Marekani waje kuwekeza na kufanya biashara
hapa nchini kutokana na fursa lukuki zilizopo.
Mhe.
Rais Magufuli pia ameiomba Marekani kusaidia kujenga hospitali kubwa ya
kitaifa katika makao makuu ya nchi Mkoani Dodoma ili kuongeza uwezo wa
Mkoa huo kutoa huduma za matibabu ikilinganishwa na ilivyo hizi sasa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam