AUAWA KWA KUPIGWA MAWE BAADA YA KUIBA KUKU MWANZA
MTU mmoja ameuawa na kundi la watu waliojichukulia sheria mkononi kwa kosa la wizi wa kuku watano wilayani Kwimba mkoani Mwanza.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed
Msangi alisema Agosti 21, mwaka huu saa tatu kasoro robo asubuhi katika
kitongoji cha Busulwa, Kata ya Ngulla Wilaya ya Kwimba, Leonard Mathias
(23), mkazi wa Kijiji cha Ngulla, aliuawa na kundi la watu
waliojichukulia sheria mkononi.
Kamanda Msangi alisema watu hao
walimpiga kwa fimbo na mawe sehemu mbalimbali za mwili wake kisha
kumchoma moto hadi kupoteza maisha kwa kosa la wizi wa kuku watano mali
ya Ester Robert ambaye ni mkazi wa kijiji hicho cha Ngulla.
Alisema, “Inasemekana kuwa mtu huyo
aliiba kuku watano nyumbani kwa Ester Robert kasha akakimbilia kijiji
cha jirani cha Mwabomba. Inadaiwa kuwa wananchi wa kijiji cha Mwabomba
walipomuona akiwa na kuku hao walipata mashaka kisha walimkamata na
baadaye walitoa taarifa Kijiji cha Ngulla ndipo mwenye kuku alifika na
kukabidhiwa kuku wake.
“Inadaiwa kuwa baada ya marehemu
kukabidhi kuku kwa mwenye mali, wananchi walimchukua na kwenda naye
kituo cha polisi, lakini wakiwa njiani walianza kumshambulia kwa kumpiga
fimbo na mawe sehemu mbalimbali za mwili wake na baadaye kumchoma moto.
Polisi walipata taarifa kutoka kwa raia
wema ndipo walifanya ufuatiliaji wa haraka hadi eneo na tukio na
kufanikiwa kukamata watu saba ambao wanadaiwa kuhusika kwa namna moja au
nyingine katika mauaji hayo,” alieleza kamanda huyo.