KIJANA AHUKUMIWA JELA MAISHA KWA KUMLAWITI MTOTO
MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala imemhukumu kutumikia kifungo cha maisha,
Erick Mbugwa (22) baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mtoto wa
miaka 14 (jina linahifadhiwa) kinyume cha sheria.
Hukumu hiyo ilitolewa jana mahakamani hapo na Hakimu Mkazi, Flora Haule
baada ya kujiridhisha na hoja za upande wa mashahidi uliowasilishwa
mahakamani hapo bila kuacha shaka yoyote.
“Mahakama inakutia hatiani baada ya kuridhishwa na ushahidi
uliowasilishwa na upande wa mashtaka ambao ulikuwa na mashahidi watano
pamoja na vielelezo vya daktari, hivyo inakuhukumu kutumikia kuifungo
cha maisha jela kulingana na kosa ulilolifanya ili iwe onyo na fundisho
kwa wengine wenye tabia kama hizi,” alisema Hakimu Flora.
Alisema iwapo mshtakiwa hajaridhika na uamuzi huo kwenye shauri hilo
namba 362 la mwaka 2016, ana haki ya kukata rufaa ndani ya siku 30.
Awali kabla ya hukumu hiyo kutolewa, Wakili wa Serikali, Chences
Gavyiole, alidai mahakamani hapo kuwa hakukuwa na kumbukumbu za mashtaka
ya nyuma dhidi ya mshatakiwa na hivyo kuiomba mahakama hiyo kutoa
adhabu kali ili iwe onyo na fundisho kwa wote wenye tabia kama hizo
kwani matendo ya namna hiyo yamekithiri kwenye jamii.
Katika utetezi wake juu ya kwa nini asipewe adhabu kali, Bugwa alidai
kuwa anaomba asamehewe kwa kuwa haikuwa ni mipango yake na huku
akisitiza kuwa hana cha kufanya na badala yake anamwachia Mwenyezi Mungu
ndiye atakayemlipia.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Mbugwa ambaye ni mkulima na mkazi wa
Chanika, anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Septemba 8 na Novemba 6,
mwaka jana maeneo ya Chanika jijini Dar es Salaam ambako alimlawiti
mvulana wa miaka 14 kinyume cha sheria.
Na FARAJA MASINDE-MTANZANIA -DAR ES SALAAM