WALIO KWENYE NDOA ZA "SOGEA TUISHI' KUPEWA ADHABU KALI

Watu wanaoishi katika mahusiano ya mume na mke bila kufunga ndoa nchini
Burundi wameamrishwa kwamba wawe wameoana rasmi ifikapo mwishoni mwa
mwaka huu la sivyo wataaadhibiwa vikali.
Msemaji wa Wizara ya mambo ya ndani na elimu Terence Ntahiraja amesema
amri hiyo itasaidia kile alichokitaja kuwa ni ongezeko la watu nchini
Burundi.
Amesema mahusiano yasiyo rasmi yamesababisha wasichana wengi wa shule
kupata ujauzito na wanaume kupata fursa ya kuwa na mahusiano ya wanawake
wengi kwa mkupuo.
Rais Pierre Nkurunziza, ambaye ni muumini wa kilokole , hivi karibuni alianzisha kampeni ya kitaifa ya maadili mema .
Burundi imekuwa katika mzozo wa kisiasa tangu mwaka 2015 Rais Nkurunziza
alipotangaza kwamba angewania urais kwa muhula mwingine.
Waziri Ntarihaja ameambia AFP kwamba ndoa zilizorasmishwa kanisani au
katika afisi ya serikali ndiyo suluhu pekee kwa tatizo la ongezeko kubwa
la watu nchini humo na kwamba ni jukumu la kizalendo.
"Tunawataka raia wa Burundi wafahamu kwamba kila mtu anawajibikia maisha
yake, na tunataka utulivu na utawala wa sheria humu nchini," alisema.
"Juhudi zote zinafanywa kwa kufuata mkakati wa kuwafunza raia wawe
wazalendo," alisema, akirejelea mpango huo wa kueneza uzalendo
uliozinduliwa na Rais Nkurunziza.
Haijabainika ni adhabu gani ambayo watapewa wale ambao hawatakuwa wamerasmisha ndoa zao kufikia mwisho wa mwaka huu.
Mkulima mmoja ameambia AFP kwamba maafisa wa serikali tayari wamemtishia
yeye na mpenzi wake kwamba watatozwa faini na kwamba mtoto yeyote
atakayezaliwa bila wawili hao kufunga ndoa rasmi hawataruhusiwa kufaidi
kutoka kwa mpango wa elimu bila malipo au huduma ya matibabu.
Mkulima huyo aliyejitambulisha kwa jina moja pekee kama Pierre, alisema
ameshindwa kuoa rasmi kwa sababu hangeweza kulipa mahari aliyoitishwa na
familia ya mpenzi wake.
Mamia ya watu walifariki tangu Bw Nkurunziza alipoanza azma yake ya kutaka kutawala kwa muhula wa tatu mwaka 2015.
Lakini miezi ya karibuni, hali ya utulivu imerejea.