TAIFA STARS YATUA SALAMA MISRI, KUANZA KUFANYA MAZOEZI USIKU
Timu ya mpira wa miguu ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inayodhaminiwa
na Bia ya Serengeti kutoka Kampuni ya Bia ya SBL, imesafiri salama
kutoka Dar es Salaam, Tanzania hadi hapa Alexandria, Misri.
Timu
iliyotumia Ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia, ilipaa kutoka Dar es
Salaam, saa 10.45 jioni ambako ilipitia Addis Ababa kuunganisha ndege ya
kufika Misri.
Stars
iliyokuwa na jumla ya watu 30 wakiwamo viongozi, benchi la ufundi na
wachezaji kwa ujumla, ilitua Uwanja wa Ndege ya Cairo, Misri majira ya
saa 7.45 usiku ambako mbali ya wenyeji Tolip Sports City, pia
ilipokelewa na maofisa wa ubalozi wa Tanzania walioko hapa Misri.
Baada
ya kupokelewa, timu hiyo ilisafiri kwa gari maalumu kutoka Cairo, Misri
hadi Alexandria umbali wa zaidi ya kilomita 180 na kufika alfajiri
baada ya mwendo wa takribani saa mbili. Saa za Misri na Tanzania zina
tofauti ya dakika 60. Misri wako nyuma kwa saa hiyo moja.
Kwa
niaba ya timu nzima, Kocha Mkuu, Salum Shabani Mayanga pamoja na
viongozi wengine akiwamo Mkuu wa Msafara, Wilfred Kidao walishukuru
Mungu kwa kusafiri salama hadi kufika hapa Alexandria kwa ajili ya kambi
ya wiki moja kujindaa kucheza na Lesotho. Pia walishukuru Watanzania
wote kwa dua zao kwa kusafiri salama.
Akizungumza
mara baada ya kukagua viwanja vya mazoezi leo asubuhi, Kocha Mayanga
ambaye alipewa majukumu ya kuifundisha timu hiyo mapema - Januari, mwaka
huu, amesema: “Programu ya mazoezi kwa timu hii itaanza leo saa 2.00
usiku. Ingawa siku nyingine nitafanya asubuhi na jioni.”
Kwa
msingi huo, alisema kesho Alhamisi Juni mosi, atakuwa na mazoezi kwa
vipindi vyote viwili uwanjani - asubuhi na usiku kabla ya kutoa
maelekezo darasani kwa siku ya Ijumaa na baadaye mazoezi ya uwanjani
tena.
Taifa
Stars inayopiga kambi hapa Misri, inajiandaa na mchezo dhidi ya Lesotho
utakaofanyika Juni 10, 2017 kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi nje
kidogo ya jiji la Dar es Salaam. Mchezo huo umepangwa kuanza saa 2.00
usiku.
Mchezo
dhidi ya Lesotho ni muhimu kwa Tanzania ikiwa ni mechi ya kwanza kwa
Taifa Stars katika Kundi ‘L’ kuwania nafasi muhimu ya kucheza fainali za
Kombe la Mataiafa ya Afrika (AFCON) za mwaka 2019 zitakazofanyika
NCHINI Cameroon.
Mbali
ya Lesotho na Tanzania, mataifa mengine katika Kundi ‘L’ ni Uganda na
Cape Verde ambao pia wikiendi ya Juni 9, 10 na 11, mwaka huu watakuwa
katika mchezo wa kwanza pia kuwania nafasi hiyo.
Wachezaji wanaounda kikosi hicho cha Kocha Salum Mayanga ni makipa Aishi Manula (Azam FC), Benno Kakolanya (Yanga SC) na Said Mohammed (Mtibwa Sugar).
Walinzi wa pembeni wako Shomari Kapombe (Azam FC), Hassan Kessy (Yanga SC), Mohammed Hussein (Simba) na Gadiel Michael.
Walinzi
wa kati ni Erasto Nyoni (Azam FC), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Abdi
Banda (Simba SC) na Nurdin Chona (Tanzania Prisons) ilihali viungo wa
kuzuia ni Himid Mao (Azam FC) na Jonas Mkude kutoka Simba SC ambaye kwa
sasa anapatiwa matibabu baada ya kupata ajali.
Viungo
wa kushambulia Salum Abubakar (Azam FC), Said Ndemla (Simba SC) na
Mzamiru Yassin (Simba) wakati viungo wa pembeni ni Simon Msuva (Yanga
SC), Shizza Kichuya (Simba SC) na Farid Mussa (Teneriffe, Hispania).
Washambuliaji
wapo Mbwana Samatta (KRC Genk- Ubelgiji), Ulimwengu (AFC Eskilstuna –
Sweden), Ibrahim Ajib (Simba SC), Mbaraka Yusufu (Kagera Sugar) na
Abdurahman Mussa (Ruvu Shooting).
Wasaidizi
wa Mayanga katika benchi la ufundi ni Novatus Fulgence ambaye ni kocha
msaidizi Patrick Mwangata - kocha wa makipa pia yumo Meneja wa timu,
Danny Msangi; Mtunza Vifaa, Ally Ruvu, Daktari wa timu ni Richard Yomba
na Daktari wa viungo ni Gilbert Kigadye.