SAKATA LA MCHANGA WA MADINI, NGOMA BADO MBICHI....CHENGE 'UKIKAA KIMYA ITALETA MANENO'
MWENENDO wa sakata la kusafirisha mchanga wa madini nje ya nchi,
umeonyesha kila dalili kwamba huenda suala hilo sasa likachukua muda
mrefu zaidi.
Tangu kamati ya wataalamu wa sayansi iliyoundwa kuchunguza kiwango cha
madini katika mchanga uliohifadhiwa katika makontena 277 yaliyoko
bandarini Dar es Salaam, iwasilishe ripoti yake, kumekuwapo na
sintofahamu ya kujua nani mkweli katika sakata hili kwa maana ya
Serikali ya Tanzania kwa upande mmoja na wawekezaji Kampuni ya Acacia
kwa upande mwingine.
Wakati ripoti iliyowasilishwa kwa Rais Dk. John Magufuli ikionyesha kuwa
kiwango cha madini kinachosafirishwa nje ya nchi ni mara kumi zaidi,
ikilinganishwa na kile ambacho kimekuwa kikielezwa, Acacia katika
matamko yao mawili waliyoyatoa wiki hii imepinga ripoti hiyo.
Acacia inadai kuwa kama kiwango hicho kinachosemwa katika ripoti ya
kamati hiyo ni kweli, basi Tanzania ni nchi inayoongoza duniani kwa kuwa
na kiwango kikubwa cha madini ya dhahabu.
Katika tamko lake la mwanzo, Acacia ambayo inachimba madini katika
migodi mikubwa ya Bulyanhulu na Buzwagi, ilieleza kuwa katika kila
kontena la mchanga kuna madini ya shaba kilogramu 3,000, dhahabu kilo 3,
na madini ya fedha kilo 3 na hivyo kufanya thamani ya kontena moja kuwa
ni Sh milioni 300.
Katika ripoti ya Kamati ya Rais Magufuli, inaeleza kuwa katika makontena
yote 277 yaliyochunguzwa dhahabu ilikuwa na uzito wa kati ya tani 7.8
na 13.16 zenye thamani kati ya Sh bilioni 676 na trilioni 1.147.
Kiwango hicho ni tofauti na makadirio ya wazalishaji na Wakala wa
Serikali wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) ambao walionyesha kuwa katika
makontena hayo, dhahabu ilikuwa ni tani 1.2 yenye thamani ya Sh bilioni
97.5 tu.
Kwa upande wa madini mengine kama fedha, katika ripoti aliyokabidhiwa
Rais Magufuli ilikuwa ni kati ya tani 1.7 na 1.9 yenye thamani kati ya
Sh bilioni 2.1 na bilioni 2.4 wakati TMAA ikidai ni kg 831 zenye thamani
ya Sh bilioni moja.
Kuhusu madini ya shaba, kamati hiyo ilibaini kulikuwa na tani 1,440.4 na
1,871.4 zenye thamani ya Sh bilioni 17.9 na bilioni 23.3.
Kiwango hicho ni tofauti na nyaraka zilizopatikana bandarini ambazo
zilionyesha kulikuwa na tani 1,108 zenye thamani ya Sh bilioni 13.6.
Kinachozua maswali na pengine baadhi sasa kuanza kuona kwamba hatima ya
sakata hilo ni mapema mno kujua mwisho wake, ni kitendo cha wadau
mbalimbali nao kuhoji uthabiti wa ripoti iliyowasilishwa kwa Rais
Magufuli.
Jana gazeti la MTANZANIA Jumamosi lilimkariri aliyewahi kuwa Mwanasheria
Mkuu wa Serikali mwaka 1993 – 2005, Andrew Chenge akihoji viwango vya
fedha vilivyokadiriwa na kamati iliyokabidhi ripoti yake kwa Rais
Magufuli.
“Lakini, ukikaa kimya italeta maneno, maana madini hayo ni mali ya
Watanzania kwani wengine wanaamini tunaibiwa na wengine hawaamini.
Wakizipiga zile hesabu na mimi ukaniambia ni trilioni, nakataa kwa
sababu ‘I know it (najua)’, nadhani kuna mahesabu wameyakosea,”
alikaririwa Chenge.
Chenge ambaye ni miongoni mwa watu wanaonyooshewa vidole na baadhi ya
wanasheria ambao wanaamini sheria na mikataba mibovu aliyoshiriki
kuiandaa wakati akiwa Mwanasheria Mkuu ndiyo kiini cha Serikali kupoteza
fedha kama ilivyoanishwa na Kamati ya Rais Magufuli, pamoja na kuhoji
huko viwango, alisisitiza kuwa suala la madini lina mambo mengi na hata
kushangaa ni kwa nini amekuwa akinyooshewa kidole.
Hoja inayofanana na hiyo ya Chenge kuhusu viwango, inaungwa mkono na
mmoja wa maofisa wa ngazi za juu ambaye alipata kufanya kazi katika
Wizara ya Nishati na Madini.
Ofisa huyo ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini kwa hoja ya
kwamba kazi yake itaharibika, aliliambia gazeti hili kuwa kamati hiyo
haikueleza ukweli juu ya usafirishwaji wa madini hayo na muda uliotumika
kuanza kusafirisha mchanga huo kwenda nje ya nchi kwa uchenjuaji.
“Kama utakumbuka mwaka 2007, Tume ya Jaji Bomani iliundwa kuchunguza
mikataba ya madini na sera ya sekta hiyo. Katika kufanya, kazi tume hiyo
iliangalia sera na sheria na mwisho ikawasilisha mapendekezo yake
serikalini kwa utekelezaji.
“Mwaka 2008, mchakato ukaanza wa kubadili sera na mwaka 2009 sera hiyo ikapatikana na mwaka 2010, tukapata sheria mpya.
“Sera hiyo ilisema tuongeze thamani ya madini kwa kujenga smelting area
(eneo la kuchenjua) kwa ajili ya kuchenjua mchanga hapa nchini na wakati
huo huo wawekezaji waelimishwe ili wajue namna ya kuomba leseni za
uwekezaji huo na namna zitakavyotolewa.
“Kuhusu hoja ya ile kamati kwamba tumekuwa tukiibiwa madini yetu kwa
miaka mingi, kamati hiyo haikuwa sahihi kwa sababu migodi inayotoa huo
mchanga ni Buzwagi na Bulyanhulu.
“Mgodi wa Buzwagi walianza kusafirisha mchanga nje ya nchi mwaka 2008 na
Bulyanhulu wao walianza mapema mwaka 2002 kama sikosei. Kwa hiyo
wanaposema tumeibiwa kwa miaka 19, sikubaliani nao,” alisema ofisa huyo.
Mrithi wa Chenge, ambaye naye alizungumza juzi na gazeti dada la
MTANZANIA Jumamosi, Frederick Werema, kauli yake kwamba haoni kama kuna
tatizo katika suala la kisheria katika mikataba ya madini, nayo imeacha
sintofahamu wakati ambapo haijulikani kamati ya wanasheria nayo itakuja
na majibu ya namna gani.
Wakati hatima ya suala hilo ikiwa bado haijulikani, hofu imetanda ya Acacia kuifikisha Tanzania katika mahakama za kimataifa.
Hofu hiyo inakolezwa na tamko lao la mwisho walilolitoa juzi, ambalo
pamoja na mambo mengine, Acacia walisema kuwa wamejipanga kutumia njia
zozote kukabiliana na jambo hilo.
Zipo hisia kwamba uamuzi wa Acacia kuitaka Serikali ya Rais Magufuli
iunde tume huru ili kuchunguza upya suala hilo, ni hatua ambayo
inaonekana kama mtego kwa Serikali ya Tanzania.
Wapo wanaoamini kuwa Acacia imefanya hivyo kwa malengo mawili, kwamba
uamuzi wowote wa Serikali kukataa ama kukubali kutekeleza jambo hilo
itakuwa ni mwanya kwao kuishtaki katika mahakama za kimataifa.
Kwamba Serikali ikikataa kuunda tume huru kitakuwa kisingizio namba moja
cha utetezi wa kuhalalisha mashtaka yao katika mahakama za kimataifa
kwa hoja kwamba tuliomba tume huru wakakataa.
Si hilo tu, inaelezwa kuwa endapo Serikali itakubali ni wazi majibu ya
tume huru yanaweza kuwa tofauti na uchunguzi wa Kamati ya Rais Magufuli
na hivyo kuipa Acacia hoja za kuipeleka mahakamani.
Kutokana na mwenendo huo na hatua ya Acacia kuomba kuundwa kwa tume
huru, Mwanasheria Victoria Mandari alisema inapotokea upande fulani
unaomba iundwe tume huru, unapaswa kueleza kwanza kama Kamati ya Rais
Magufuli haikuwa huru.
Katika muktadha huo, alisema hawezi kukanusha au kusema chochote kwa
sababu hajafanya utafiti wa kubaini kama kamati hiyo haikuwa huru au la
kwa kuwa anajua utaratibu wa kamati hufanya kazi kwa maelekezo
iliyopewa.
“Kuna suala la usiri pamoja na kufuata hadidu za rejea walizopewa, sasa
kama walizingatia hayo na wewe huamini, basi tuambie wazi kwamba kamati
haikuwa huru na kama ni hivyo inabidi utueleze haikuwa huru kwa kiwango
gani na ili iwe huru ilitakiwa kuwaje. Je iliingiliwa? Je, kuna mkono wa
mtu?
“Kwa sababu ili uweze kuhitaji tume huru, unatakiwa uwe umefanya utafiti
na umepata majibu ya uhakika ambayo yanapinga ripoti ya uchunguzi wa
kamati,” alisema.
Naye Jaji mstaafu, Amir Manento, alisema hawezi kuzungumzia masuala ya madini kwa sababu hana utaalamu wowote kuhusu madini.
Alisema anaamini kuwa kinachosikika kwa sasa nje ya ripoti iliyokabidhiwa kwa Rais Magufuli ni mambo ya kubuni tu.
“Nami nimekuwa ni msikilizaji wa haya yanayozungumzwa kwa sasa baada ya
ripoti kukabidhiwa kwa Rais. Najua yanayoongelewa ni masuala ya kubuni
tu, kwa sababu neno labda limetawala, hata nyinyi watu wa magazeti
mnaandika labda akina fulani matumbo joto na kadhalika.
“Yamekuwa ni mawazo ya watu binafsi ndiyo yametawala, kwa hiyo hata mimi
sitaki kutoa mawazo yangu kwa kitu ambacho siwezi kuthibitisha. Kwa
ujumla haya tunayoyasikia kwa sasa hayapo kwenye msingi wa sheria ila ni
akili ya kawaida,” alisema Jaji Manento.
Katika hatua nyingine, Jaji Manento alihoji maana ya tume huru huku akimtaka mwandishi awaulize Acacia watoe tafsiri halisi.
“Nasikia tume huru, hivi ni nini? Binafsi sijawahi kujihusisha na tume
yoyote ile ambayo inasemwa ni huru au si huru. Sasa hao wanaosema
wanataka tume huru waulizeni kwamba wanamaanisha nini,” alisema Jaji
Mane