Kocha
Mkuu wa Singida United, Mholanzi, Hans van Der Pluijm, amesema hakuna
mazungumzo yoyote yanayoendelea kati yao na wachezaji wa Simba, kiungo
Jonas Mkude na mshambuliaji, Ibrahim Ajibu.
Pamoja
na Pluijm kutotaka kuweka mambo yote hadharani lakini kuna taarifa
tayari kuna jambo dhidi ya nyota hao wa Simba na kuna dau limeandaliwa
kuwashawishi.
Wachezaji
wengine wanaotajwa kusajiliwa na Singida msimu ujao wa ligi kuu ni
Atupele Green anayekipiga Ndanda FC na kiungo fundi wa Yanga,
Mnyarwanda, Haruna Niyonzima.
Pluijm
amesema muda wa usajili bado, hivyo ni mapema kuzungumzia katika
kipindi hiki na hizo taarifa zinazoenea za kumsajili Mkude na Ajibu ni
tetesi pekee.
Pluijm
alisema, bado hajaanza kazi rasmi ya kukisuka kikosi hicho na mara
atakapoanza, basi haraka ataweka wazi mipango yake yote ikiwemo ya
usajili. Hata hivyo, tayari usajili wa Singida United umeanza na
wameshanasa takriban nyota watatu wakiwemo wa kimataifa.
"Ujue
nimeikuta Singida ikiwa tayari ina wachezaji ambao wameipandisha
kucheza ligi kuu, hivyo ni lazima niwape nafasi hawa niliowakuta kwanza
kabla ya kuanza usajili wa wachezaji wapya.
"Na
kingine mimi bado sijaanza kazi rasmi, hivyo nisubirie tuanze kwanza,
halafu kila kitu ntakwambia, ni ngumu kuweka mipango yangu nikiwa bado
sijaanza kazi.
"Hizo
taarifa za kuwasajili wachezaji hao bado siyo rasmi, ni tetesi pekee,
licha ya kutoa mapendekezo kwa uongozi wangu," alisema Pluijm.