Benki ya NMB
imetoa elimu ya masuala ya kibenki na umuhimu wa kujijengea utamaduni wa
uwekaji akiba kwa wanafunzi na baadhi ya wazazi wa Shule ya Msingi
Wailes iliyopo Temeke jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na
wanafunzi wa Shule ya Msingi Wailes walioshiriki mafunzo hayo ya
kifedha, Ofisa wa Benki ya NMB Tawi la Temeke, Latifa Ayoub Dadah
alisema NMB inaendelea kutoa elimu ya masuala ya kifedha ikiwa ni pamoja
na kujifunza mbinu za kuweka akiba kwa ajili ya maisha ya baadae.
Alisema elimu
hiyo inatolewa kupitia Programu maalum ya Wajibu ambayo hutoa fursa kwa
watoto, vijana na wazazi kujifunza masuala ya kifedha ili kumjengea
mtoto utamaduni wa kujiwekea akiba, elimu ambayo watoto wengi hawapati
fursa ya kujifunza.
Akizungumza
katika mafunzo hayo, alisema vijana wengi wamekuwa hawana utaratibu wa
kujiweka akiba tangu wadogo hivyo NMB kupitia programu ya Wajibu
inaendelea kutoa elimu kwa watoto, vijana pamoja na wazazi wao kuelewa
umuhimu wa kujiwekea akiba ya fedha kupitia akaunti mbali mbali za benki
hiyo, kama vile Mtoto Account, Chipukizi Account na Mwanachuo Account.
NMB katika
ziara hiyo ambapo ilikuwa imeongozana na wachezaji wa Timu ya Mpira wa
Miguu ya Azam kupitia kituo chao cha michezo, mbali na anafunzi na
wazazi kupata elimu ya masuala ya kifedha na uwekaji akiba kwa manufaa
ya baadaye, wachezaji wa Azam walicheza mpira na wanafunzi hao pamoja na
kugawa zawadi mbalimbali toka NMB na kampuni ya Azam.
Akifafanua
zaidi, Bi. Latifa alisema elimu hiyo ni mwendelezo wa programu ya wajibu
ambapo NMB imekuwa akizunguka katika shule mbalimbali za msingi na
sekondari nchi nzima huku ikitoa elimu ya kifedha na masuala mazima ya
uwekaji akiba.
"...Mwitikio
kwa waliopata fursa ya kushiriki katika mafunzo haya ni mzuri kwa kwli
hasa katika wilaya yetu ya Temeke, tumekuwa tukipokea watoto mbalimbali
wakija kufungua akaunti jambo ambalo linaonesha wamevutiwa na elimu
hii," alisema ofisa huyo wa Benki ya NMB Tawi la Temeke.
Naye Mwalimu wa
Taaluma wa Shule ya Msingi Wailes, Zabibu Wasia aliishukuru Benki ya
NMB kwa kutoa mafunzo hayo kwa wanafunzi pamoja na baadhi ya
wazazi/walezi wa shule hiyo na kuahidi kuendelea kuwa mabalozi kueneza
elimu hiyo kwa wengine kutokana na umuhimu wake. "..Tunaishukuru sana
NMB kwa kuamua kuleta elimu hiyo kwa wanafunzi na wazazi wa Wailes
tunaamini hii ni fursa ya kipekee kwetu maana shule za msingi Dar es
Salaam zipo nyingi lakini umeona muanze na sisi...tunashukuru sana kwa
kutupendelea," alisema Bi. Wasia.
Mbali na elimu
hiyo NMB ilitoa mipira miwili kama zawadi kwa wanafunzi wa Shule ya
Msingi Wailes, yaani mpira wa miguu kwa wanafunzi wa kiume na mpira wa
pete kwa wanafunzi wa kike.