MKOA WA MARA WACHAGULIWA KUWA MWENYEJI WA MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI.
Mkuu wa
Mkoa wa Mara, Dk Charles Mlingwa, akizungumza na waandishi wa habari Mkoani
Mara jana kuhusiana na mkoa huo kuwa mwenyeji wa siku ya mazingira.
****************
MKOA wa mara umechaguliwa kuwa mwenyeji wa Siku ya
mazingira duniani ambapo kitaifa itaadhimishwa kitaifa mkoa wa Mara katika
Wilaya ya Butiama kuanzia Juni 1-6 mwaka huu.
Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira,
Januari Makamba anataraji kufungua maadhimisho hayo na Makamu wa Rais, Samia
Suluhu Hassan anataraji kuwa mgeni rasmi katika kilele chake.
Maadhimisho hayo yatafanyika katika uwanja wa Mwenge Mjini
Butiama ambapo kutakuwapo na kongamano na tafrija mbalimbali kuhusiana na
maswala ya mazingira.
Mkuu wa mkoa wa Mara, Dk Charles Mlingwa alisema kuwa
katika siku hiyo ya mazingira inategemewa kupandwa miche ya asili 1,500 ya miti
katika misitu mbalimbali eneo la Butiama kama ilivyo kawaida ya maadhimisho
hayo.
Aidha Dk Mlingwa amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi
ili kujumuika pamoja kwenye maadhimisho hayo muhimu ambayo yatafanyika mkoani
Mara kwa mara ya kwanza.
Mbali na hapo Mlingwa alisema kuwa wananchi watapata faida
katika maadhimisho hayo kama kuijengea jamii uwezo juu ya uelewa wa masuala ya
mazingira na changamoto za kijamii zinazojitokeza katika utunzaji wa mazingira
na kuwezesha wadau kushiriki katika fursa zinazohusiana na upandaji wa miti.
Pia watapata fursa ya kujadili mwendelezo wa utekelezaji
wa shughuli zilizoratibiwa katika mkoa na wizara kuhusu namna bora ya uhifadhi
wa mazingira na kuenzi kazi zote za Baba wa Taifa Mwal. Julius Nyereree katika
hifadhi ya mazingira.
Mlingwa alisema kuwa wataelimishwa kupanda miti ili
kukidhi mahitaji ya dunia ya kupambana na ongezeko la hewa ya ukaa.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Hifadhi mazingira muhimili wa
Tanzania ya viwanda” ikiwa na maana ya ulinzi na uhifadhi wa mazingira nchini
kuleta maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii.