MANGU : POLISI,WANANCHI MPENI USHIRIKIANO IGP SIRRO
Aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu amewataka
wananchi kumpa ushirikiano IGP mpya, Simon Sirro katika kukabiliana na
matukio ya uhalifu nchini hasa katika Mkoa wa Pwani.
Mangu aliyasema hayo jana Ikulu jijini Dar es salaam baada ya Rais John
Magufuli kumwapisha Sirro kuwa IGP mpya wa kuliongoza jeshi la polisi
nchini.
Kuhusiana na hali inayoendelea mkoani Pwani, Mangu alisema "Sirro
anafahamu anachotakiwa kufanya katika hilo, nimefanya naye kazi kwa
karibu, ninachoomba ni askari na wananchi wote wampe ushirikiano"
Mangu ambaye anasubiri kupangiwa kazi nyingine alisema anamfahamu Sirro
kama mchapakazi mzuri na ataweza kutekeleza majukumu yake ya kuhakikisha
kwamba Tanzania inakuwa na amani.
Sirro aliapishwa jana kuwa IGP, kabla ya uteuzi huo alikuwa kamanda wa polisi (RPC) katika mikoa ya Tanga, Mwanza na Shinyanga.
Baadaye alikwenda kitengo cha operesheni na mafunzo polisi makao makuu,
kisha akahamishiwa kitengo hicho kanda maalumu ya Dar es Salaam kabla ya
kuwa kamishna wa kanda hiyo.