KUMEKUCHA AZAM FC NA BOCCO, YAELEZWA AMERUHUSIWA KUONDOKA, YEYE ATUPIA MANENO MTANDAONI, AZAM WATOA UFAFANUZI
Taarifa za nahodha wa Azam FC na mshambulizi tegemeo, John Bocco kuwa ametemwa Azam FC zimeenea kila sehemu mitandaoni.
Kumekuwa na taarifa kwamba Azam FC wameamua kuachana na Bocco ambaye ameichezea timu hiyo tokea ianzihwe.
Ambacho
kinaonekana kuwashitua mashabiki ni Bocco kutupia maneno kadhaa
mtandaoni ya kijamii katika akaunti zake yanayoashiria kuaga au
kuondoka.
Hata hivyo, SALEHJEMBE imefanya juhudi na kupata uhakika kutoka ndani ya Azam FC na kugundua kuwa mkataba wa Bocco umemalizika.
“Ni kweli mkataba wa Bocco umeisha na sasa yuko katika mazungumzo na uongozi.
“Suala la kwamba anaondoka sijalisikia, lakini najua wanazungumza,” kilieleza chanzo.
Juhudi za kumpata Bocco, kumekuwa na ugumu lakini alipatikana Msemaji wa Azam FC, Jaffar Iddi ambaye naye alitoa ufafanuzi wake.
“Suala la mchezaji kuingia katika mazungumzo na klabu ni la kawaida.
“Kuhusu mkataba wake na klabu inabaki kuwa siri ya hizo pande mbili lakini hakuna taarifa za Bocco kuachwa,” alisema.