Nahodha
na mshambuliaji wa Azam, John Bocco, ameweka bayana kuwa kadi nyekundu
aliyopata kiungo wao, Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ ndiyo ilichangia kwa
kiasi kikubwa wao kupoteza mechi yao na Simba kutokana na kulazimika
kubadilisha mbinu ambazo zilisababisha washindwe kuipenya safu ya ulinzi
ya wapinzani wao hao.
Kiungo
huyo, Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ alipewa kadi nyekundu dakika ya 16 ya
kipindi cha kwanza na mwamuzi Mathew Akrama wa Mwanza kabla ya Mohammed
Ibrahim ‘Cabaye’ wa Simba kupewa kadi nyekundu dakika ya 76.
Azam
inayonolewa na Mromania, Aristica Cioaba, juzi Jumamosi iliondoshwa
katika michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) baada ya kufungwa na Simba
kwa bao 1-0 katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar.
Bocco
amesema kuwa Sure Boy ndiye aliyewagharimu kwa kiasi kikubwa kutokana
na kadi yake hiyo ambapo iliwalazimu kubadilisha mfumo waliokuwa
wakiutumia na kusababisha kushindwa kutengeneza nafasi za kuifunga timu
hiyo.
“Tulianza
vizuri na tuliwabana Simba lakini baada ya Sure Boy kupata kadi
nyekundu kila kitu kwetu kilibadilika na kutulazimu kucheza kwa
tahadhari na hata mashambulizi tuliyokuwa tunayapanga yakafa kwa sababu
ya kuhofia kufungwa maana tulikuwa pungufu.
“Hatuna
la kufanya kwani tushatolewa kwenye mashindano haya na pia hatuna kitu
chochote cha kugombea zaidi ya kupigania kumaliza kwenye nafasi za juu
kwenye ligi na kujipanga kwa ajili ya msimu nujao,” alisema Bocco.