BARTHEZ, JOSHUA SAFARI YAO YANGA IMEISHIA MSIMU HUU, SINGIDA YAWANYATIA
Kipa
mkongwe wa Yanga, Ally Mustapha 'Barthez' na beki wa pembeni wa timu
hiyo, Oscar Joshua ni kati ya wachezaji watakaokuwepo kwenye kikosi cha
Singida United katika msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
Kama hawatakuwa katika kikosi hicho basi safari yao kwa upande wa Yanga itakuwa imeishia hapo.
Barthez
na Joshua ni kati ya wachezaji ambao hawakuwa na nafasi ya kucheza
katika kikosi cha kwanza cha Mzambia, George Lwandamina katika msimu
uliopita wa ligi kuu.
Wachezaji hao wote bado wana mikataba ya mwaka mmoja wa kuichezea Yanga kwenye msimu ujao wa ligi.
Kwa
mujibu wa taarifa za ndani wachezaji hao wataondolewa Yanga na
kupelekwa Singida inayofundishwa na Kocha Mkuu Mholanzi, Hans Pluijm
aliyekuwa anaifundisha timu hiyo kabla ya nafasi yake kuchukuliwa na
George Lwandamina.
Mtoa
taarifa huyo alisema, wachezaji hao walikuwepo kwenye orodha ya
wachezaji watakaochwa katika msimu ujao, lakini kutokana na mikataba yao
kutomalizika watapelekwa kwa mkopo.
"Barthez
na Joshua hawana nafasi ya kucheza katika kikosi cha Lwandamina na pia
hana mipango nao, hivyo kama uongozi tumeona tuwatoa kwa mkopo.
"Tutawatoa
baada ya kufanya mazungumzo na uongozi wa Singida na kukubali
kuwachukua, hivyo tumeona tuwaachie waende huko wakacheze,"alisema mtoa
taarifa huyo.
Alipotafutwa
Barthez kuzungumzia hilo alisema kuwa ":Bado sijapata taarifa rasmi ya
kupelekwa kwa mkopo, ni tetesi ninazozisikia pekee kama ulivyosikia wewe
ni vema tukasubiria kwanza kabla ya mimi kuongea chochote.
"Kingine
ni ngumu mimi kuondoka kabla ya kupelekwa huko na Yanga, kama unavyojua
bado nina mkataba wa kuichezea Yanga,"alosema Barthez.