Na Husna Saidi
Wazazi na walezi wametakiwa kutoa
kipaumbele cha elimu kwa watoto wakike kutokana na Serikali kutoa fursa ya
elimu bure kwa shule za Msingi na Sekondari ili kuongeza usawa wa kijinsia katika
elimu.
Hayo yamesemwa na Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati
akifungua Kongomano la kwanza la Kimataifa la Kijinsia lililoandaliwa na Chuo
Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) ambapo alimwakilisha Makamu wa
Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan leo Jijini Dar es Saalam.
Waziri
Ummy alisema kuwa uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Tano kutoa elimu bure unatoa fursa zaidi kwa mtoto wa kike kunufaika
na elimu tofauti na awali ambapo kutokana na hali ya maisha kuwa duni familia
nyingi zilitoa kipaumbele kwa mtoto wa
kiume na kuwaacha wakike kufanya shughuli za nyumbani.
“Niwaombe
wataalam wetu tuungane kwa pamoja kuhakikisha watoto wa kike wanapewa fursa
sawa katika kujiunga na masomo, ata waliopata mimba kwa bahati mbaya wapewe
fursa ya kurudi mashuleni,” alisema Waziri Ummy.
Aidha
aliongeza kuwa ili kuleta asilimia hamsini kwa hamsini kwa wote wazazi wanatakiwa
kuwahamasisha watoto wakike kupenda masomo ya Sayansi kwani inaonesha watoto
wengi wakike hawana hamasa na masomo hayo.
Aidha
aliupongeza uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa kuweza
kufanikisha kuwa na wanafunzi wakike asilimia 38 wakati Serikali imefanikisha
asilimia 32 ya wanafunzi wakike katika elimu ya juu.
Kwa
upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa Rwekaza
Mukandala alisema kuwa tangia mwaka 1993 kulikuwa na mikakati ya kuwaweka
watoto wa kike katika fani mbalimbali na kuwapa ujuzi ambapo imeonesha watoto
wengi wa kike walikuwa wanaongoza kwa kufanya vizuri zaidi.
Nae
Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) Profesa William
Anganisya alisema kuwa Kongamano hilo litaonesha nafasi ya mwanamke katika
jamii na kuwa chachu kwa watoto wakike kupenda masomo ya Sayansi.
Serikali
imejipanga kuja na mikakati mipya madhubuti ya kuboresha idadi ya wanafunzi wa
kike hasa katika elimu ya juu ili kuleta usawa wa kijinsia.