ULIISIKIA HII YA MANJI KUWAIBUKIA MAZOEZINI WACHEZAJI WA YANGA?
Mwenyekiti
wa Klabu ya Yanga, Yusuf Manji, juzi Jumatano kwa mara ya kwanza baada
ya muda mrefu alitinga kwenye mazoezi ya timu hiyo na kuzungumza na
wachezaji wote waliopanga kugoma kushinikiza kulipwa mishahara yao
wanayodai kwa miezi mitatu.
Manji
ambaye kwa muda mrefu amekuwa kimya kutokana na matatizo binafsi
yanayomkabili, alilazimika kufanya hivyo ikiwa ni siku moja kabla ya
kikosi hicho kusafiri kwenda Algeria kupambana na MC Alger katika mchezo
wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika utakaopigwa kesho Jumamosi.
Mazoezi hayo ya mwisho yaliyofanyika Uwanja wa Taifa, Dar, yalichelewa kuanza kwa saa 1:15 kutokana na kuwepo kwa mgomo huo.
Kikao
chao kilianza saa 10:00 jioni hadi saa 11:15 walipoanza mazoezi huku
Mzambia, Obrey Chirwa na Wazimbabwe, Thabani Kamusoko na Donald Ngoma
wakigoma kabisa kufanya mazoezi baada ya kufika wakiwa na mavazi yao ya
nyumbani tofauti na wenzao waliovalia mavazi ya mazoezini.
Wakati wa kikao bosi mmoja wa benchi la ufundi alisikika akiwabembeleza wachezaji kuvumilia hali iliyopo klabuni kwao kwa sasa.
Bosi huyo aliwaambia Manji ameomba muda wa miezi miwili kuweka mambo yake sawa.
Wakiwa
kwenye mazungumzo ya mwisho pamoja na kuomba dua kabla ya kuondoka
uwanjani hapo, ghafla Manji akaingia akiwa na watu watatu na moja kwa
moja akajumuika nao na kuanza kuongea kwa takribani dakika nane, kisha
akaondoka.
Baada
ya Manji kuondoka, katibu wa klabu hiyo, Charles Mkwasa, akaanza
kuzungumza na wachezaji hao kwa nusu saa, baada ya hapo wakatawanyika
huku wachezaji wakionekana kuwa na furaha tofauti na awali.
Taarifa
ambazo zilipatikana baadaye baada ya wote kutawanyika, ni kuwa
waliahidiwa kulipwa fedha zao kuanzia jana kitendo ambacho kiliwafanya
baadhi ya wachezaji kumvaa Mkwasa na kuanza kumuuliza utaratibu wa
kuzipata fedha hizo.
Mkwasa akawapa maelekezo yote ya namna ya kupata fedha zao.
Alipofuatwa
Mkwasa kutaka kujua walichokuwa wakikijadili baada ya Manji kufika
mazoezini na mambo mengine, lakini hakuwa tayari kutolea ufafanuzi.
SOURCE: CHAMPIONI