STAA CHIRWA AWAZIMIA SIMU VIGOGO WA YANGA, WAHAHA KUMPATA
Pamoja na juhudi za vigogo wa Klabu ya
Yanga kumshawishi mshambuliaji wao, Obrey Chirwa raia wa Zambia kuungana
na wenzake kuelekea nchini Algeria kuwavaa MC Alger ya nchini humo,
taarifa kutoka ndani ya viongozi hao ni kuwa mshambuliaji huyo
hakupatikana hewani baada ya kufunga simu zake zote.
Chirwa aliyejiunga na Yanga mwanzoni mwa
msimu huu akitokea FC Platinum ya Zimbambwe, aligoma kuungana na
wenzake kwa ajili ya safari hiyo kwenye mchezo wa marudiano wa Kombe la
Shirikisho Afrika dhidi ya MC Alger kwa kile kinachodaiwa kutokulipwa
kwa mishahara yake ya miezi mitatu.
Habari za uhakika ni kuwa baada ya
Chirwa kugoma ndipo jina lake likaondolewa katika orodha ya waliotakiwa
kusafiri kwenda Algeria, jana jioni.
“Jana (juzi) kuna vigogo wa Yanga ambao
sitapenda kuwataja majina yao walikuwa wakimtafuta Chirwa ili
kumshawishi aungane na wenzake katika safari lakini simu zake zote za
mkononi zilikuwa hazipatikani,” kilisema chanzo na kuendelea:
“Kuna waziri alinipigia simu akiniulizia
ishu hiyo nikamueleza mimi ninavyojua, hivyo akaniomba nimtafute Chirwa
ili aweze kuzungumza naye ikiwezekana aungane na wenzake ila
imeshindikana maana nilimpigia Chirwa sikumpata, nilipoenda nyumbani
anapoishi sikumkuta.”
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa, alisema: “Chirwa hajaungana na wenzake kwa kuwa ana matatizo yake ya kifamilia.”