SAFARI YA SIMBU BUNGENI IKO HIVI, DSTV YAENDELEA KUWA NAYE BEGA KWA BEGA
Mwanariadha
nyota nchini, Alphonce Simbu aliyeshika nafasi ya tano katika
mashindano ya London Marathon, jana Alhamisi alitembelea Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kupata mwaliko maalum wa Waziri
wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Harryson Mwakyembe.
Akizungumzia
mwaliko huo, Simbu amesema: “Nimefurahi sana kupata mwaliko huu kwani
inaonyesha ni kwa kiasi gani serikali inafanya jitihada za kutambua
jitihada tunazofanya vijana wao katika kuliletea taifa sifa.”
Kwa
upande wake, Meneja Uhusiano wa Multichoice Tanzania ambao ndiyo
wadhamini wakuu wa mwanariadha huyo kupitia king'amuzi chao cha DSTV,
Johnson Mshana, amesema kuwa mwaliko huo unatoa picha kwamba serikali
ipo karibu na watu wake, lakini pia itaimarisha kuendeleza michezo hapa
nchini.
Multichoice
Tanzania kupitia DSTV, imekuwa ikimdhamini Simbu tangu mwaka jana na
udhamini huo pia umewanufaisha wanariadha wengine ambao wamekuwa kambini
kwa muda sasa pamoja na Simbu.
Alphonce
Simbu, ambaye pia ni mshindi wa medali ya dhahabu katika mashindano ya
Mumbai Marathon yaliyofanyika mwanzoni mwa mwaka huu nchini India, ni
miongoni mwa wanariadha wa timu ya Taifa itakayoshiriki mashindano ya
dunia yatakayofanyika jijini London, Agosti, mwaka huu.