MANARA AMEUMIZWA NA KANUNI ZA KITWANA UENDESHAJI LIGI KUU BARA, ZINAWALINDA MABWANA



Na Saleh Ally
TUNAKWENDA taratibu na mnaanza kunielewa, ninaamini hivyo. Sitajali kwamba nawakasirisha wachache wanaofaidika lakini nataka kuendelea kusema ukweli.


Sisi wote ni wadau wa soka, lakini nataka tuwe watu huru wenye uwezo wa kutafakari na kuona tuendako kwa kuwa mpira wa Tanzania ni mali ya Watanzania.


Nitawakumbusha, unaposikia Shirikisho la Soka Tanzania, yaani TFF, hii ni mali yako wewe Mtanzania na wale walio pale wamepewa dhamana kupitia wewe, sema mfumo wa uchaguaji watu ni duni, na umetengenezewa misingi duni ili kuweza kuwapenyeza hata walio na uwezo mdogo sana wa kuongoza.


Nitajikita kwenye kanuni, hasa baada ya juzi kufungiwa kwa Msemaji wa Simba, Haji Sunday Manara, kijana ambaye alikuwa anapigania klabu yake. Akaona kuna kasoro akasema anachoamini ni sahihi.

TFF kama nilivyosema tumewapa dhamana, wao ndiyo wasimamizi. Wakaona hayuko sawa na kuchukua hatua. Nafikiri ni sehemu ya usimamizi na wana haki ya kusimamia.


Lakini usimamizi wao uko sahihi? Ni ule unaotoa haki kwa watu wote? Haya ni mambo ya kujiuliza na lazima ujue TFF wanatoa adhabu zao kupitia kanuni ambazo wameziunda na wameziboresha wao. Niwe wazi hapa kanuni ziko kwa ajili ya kuwalinda walio madarakani na zimekuwa na makali sana kwa kuwa walio madarakani hawajiamini kutokana na udhaifu wa kiuwezo, lazima wajilinde.


Kanuni za Ligi Kuu Bara za mwaka 2016 ndiyo zilizomhukumu Manara. Ni kanuni zinazoonyesha udhaifu, kuna kanuni zilizokaa kitwana kwa ajili ya mabwana.
Manara alipatikana na hatia mara tatu: (1), kukashifu, (2), ilielezwa kuzungumza lugha inayohusu ukabila na (3) kuiingilia kamati.

Kosa la kwanza ni kufungiwa miezi 12 na Sh milioni moja. Kosa la pili kalimwa faini ya Sh milioni tatu na mwisho kuingilia kamati akalambwa faini ya Sh milioni 5. Hii ndiyo ile ambayo Dk Damas Ndumbaro alikutana nayo akafungiwa kwa miaka saba.


Hii kanuni iliyotoa adhabu ya tatu ni kipengele cha 41 (16) ambayo inaeleza hivi: “Akibainika kushawishi, kupotosha au kuzuia maamuzi/utekelezaji wa maamuzi ya TFF/TPLB, atatozwa faini ya Sh 5,000,000 na/au kufungiwa kujihusisha na masuala ya mpira wa miguu kwa kipindi cha miaka saba.”


Nataka nikuulize wewe mdau, kweli TFF kama imeamua jambo halafu ukaona lina kasoro na wewe ni mdau au kiongozi wa soka, umeamua kulikemea au kusema si sahihi, hili ni jambo baya? Nani kati yetu anaamini TFF itakuwa ikifanya mambo yake yote bila kukosea hata kidogo?


Unaona moja ya kanuni ambazo zimetengenezwa kuwaogofya wadau wa soka, au kuwaadhibu wale wanaoonekana kuwa tofauti na mabwana. Ndiyo maana nikaziita kanuni za kitwana.


Kweli bila ya woga, aliyetoa hisia zake dhidi ya TFF, huenda zina makosa sawa. Je, anastahili adhabu ya faini ya Sh milioni 9? Hii ni kukomoana kwa wazi, wakati ule Jamal Malinzi akiwa katibu mkuu wa Yanga, mara nyingi tu aliikosoa TFF katika mambo kadhaa akiitetea klabu yake.

Hali kadhalika, Mwesigwa Selestine alizungumza kauli kupinga mambo kadhaa ambayo aliamini si sahihi. Ninaamini hawakufanya jambo baya kwa kuwa wao ndiyo familia ya soka na walikosoa ili kufikisha maoni kama wadau na kusaidia marekebisho.


Hizi kanuni zilizo sasa, hatukuona akina Leodegar Tenga na wengine wakizishadadia. Sasa imekuwa too much. Nilianza kusema kwa Dk Ndumbaro, nikawakumbusha tena kwa Jerry Muro, sasa imehamia kwa Manara na nasisitiza, hili litaendelea ili kuendelea kujenga ngome imara ya wale “wasioguswa”, jambo ambalo si sahihi hata kidogo.

Unajua mfumo wa mabwana na watwana, hatupaswi kuutumia kutafuta maendeleo ya jambo. Mashirikisho na vyama vya soka vilivyoendelea barani Ulaya na kwingineko, vinakosolewa, vinahojiwa na wakati mwingine vinakataliwa. TFF ni nani na imefanya nini kikubwa zaidi ya kuendelea kutuangusha miaka nenda rudi? Inajivunia kipi hadi ikatae kukosolewa?


TFF inajua, kwa msimu huu zaidi ya mechi 20 zimechezwa hazikuwahi kuingiza kiingilio cha jumla Sh milioni 9. Leo, mtu kwa kusema tu anapigwa faini ya kiasi hicho, hii si haki. TFF wanajua hata wao kuwa wanaingiza kiasi gani kupitia mpira na wanaowapa adhabu wajue ni watu wa mpira.

Si sahihi kuendelea kujengeana hofu na kutengeneza familia ya watu waoga ili wawaache viongozi wa TFF wafanye wanavyotaka bila kuguswa.


Hizi kamati zilichaguliwa na uongozi wa juu wa TFF. Zinafanya maamuzi zikiitwa kamati huru lakini kila kitu kinaonyesha ni kutimiza furaha ya waliozichagua.


Waungwana acheni ushabiki, acheni uonevu na ndiyo maana sasa kwenye kuichangia Serengeti Boys mnataka watu waungane na hii ni kwa kuwa TFF haina fedha na inapambana. Naunga mkono ni jambo zuri lakini vizuri muungane na wadau hata siku msipokuwa na shida.


Acheni ubabe usio na sababu za msingi, acheni kuharibu mpira kwa maslahi yenu binafsi. Bado Manara angeweza kuonywa na hata kama ni kuadhibiwa, si adhabu hizi mlizotoa ambazo zinaonyesha wazi, mnataka kuogopwa ili mfanye mnavyotaka. Haitawezekana kwa kuwa TFF ni ya Watanzania, ni lazima mbadilike.

SOURCE: CHAMPIONI
Powered by Blogger.