Makamu wa Rais Mgeni Rasmi Kongamano la Kimataifa la Jinsia
Na Husna Saidi
Makamu
wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Kongamano
la Kimataifa la Jinsia na Usawa Katika Jamii
lililoandaliwa na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) Aprili
27 mpaka 28 mwaka huu chuoni hapo.
Hayo
yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Afisa Habari, Elimu na Mawasiliano wa Chuo
hicho Lila Mandu alipokuwa akiongea na
waandishi wa habari kuhusu lengo la kongamano hilo.
Mandu
alisema lengo kuu la kongamano hilo ni kuchunguza kwa kina masuala mbalimbali
ya kijinsia pamoja na kubaini mbinu bora za kuondoa ukosefu wa usawa wa jinsia katika
muktadha wa Taasisi za Elimu ya Juu.
“Tutatathmini
sababu na changamoto zinazosababisha ukosefu wa usawa wa kijinsia katika
Taasisi za Elimu ya Juu kwa kutumia mifano mizuri kutoka Taasisi zingine ambazo
zinajitahidi kuhamasisha usawa na haki za wanawake na wanaume pia,” alisema
Mandu.
Aliendelea
kwa kusema kuwa kongamano hilo litabainisha fursa za kimkakati katika
kuwahusisha wadau wa masuala ya jinsia katika kuhamasisha usawa na haki za watu
wote ambapo litakuwa na washiriki 140.
Aliwataja
washiriki hao kuwa ni wasomi kutoka DUCE, Taasisi na vyuo mbalimbali ndani na
nje ya nchi, wanafunzi wa shahada za uzamili na uzamivu katika masuala ya
jinsia, wawakilishi wa mashirika ya haki za binadamu, watunga sera pamoja na
wasomi wanaotambulika Kimataifa katika masuala ya jinsia.
Kwa
upande wake, Mratibu Kitengo cha Jinsia DUCE Fatma Hamad alisema licha ya maovu
wanayotendewa wanawake kuendelea kujitokeza hapa nchini, kongamano hilo
litasaidia kutoa elimu ya jinsia na usawa ili kusaidia Serikali na wananchi kwa
ujumla kuondokana na hadha hiyo.
Chuo
cha DUCE pamoja na waandaaji wa kongamano hilo wamealika wadau mbalimbali wa masuala
ya jinsia, wasomi, waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla kushiriki katika
kongamano hilo.