MADIWANI KAHAMA WATAKA SEKONDARI ILIYOTUMIA MIAKA 11 KUJENGWA IKAMILIKE
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kahama,Abel Shija |
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Mji
wa Kahama mkoani Shinyanga,wameamuru kukamilishwa mara moja kwa ujenzi
uliotumia miaka 11 katika Shule ya Sekondari Kitwana,iliyoko Kata ya
Busoka,ili kunusuru wanafunzi
Maazimio ya Baraza hilo yalifikiwa juzi,baada ya Diwani wa Kata ya
Busoka,Julius Malale,kuwasilisha malalamiko ya wananchi wa Kijiji cha
Kitwana,wanaohitaji kurejeshewa maeneo yao waliyoyatoa kwa ajili ya
ujenzi wa shule ya sekondari Kitwana,ambao umeshindikana kukamilika.
Katika malalamiko hayo,Wananchi hao wamedai hawaoni faida ya kuyatoa
maeneo hayo na kuhitaji kurejeshewa,kutokana na kutokamilika ujenzi wake
kwa miaka 11,huku Shule nyingine zilizoanza ujenzi wake hivi karibuni
zikikamilika,ilhali vijana wao wakiendelea kuteseka kutembea umbali
zaidi ya kilometa 15 kufuata shule katika kata jirani.
“…kuna shule zilizoanza ujenzi na Kitwana zimekamilika na kuanza
kutumika,zingine ujenzi wake umeanza hivi karibuni nazo zinafanya
kazi,sasa wana kijiji hao waliotoa maeneo hayo wanadai leo ni miaka
11,imeshindikana kumaliza ujenzi huo wa sekondari,warejeshewe maeneo
yao,kwani hayana tija tena kwa elimu,” alisema Malale.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kahama mjini,Hamidu Kapama,aliliambia
baraza hilo kutokamilika ujenzi kwa sekondari hiyo,ni uzembe
uliosababishwa na halmashauri kupitia afisa elimu sekondari kwakuwa
serikali imekuwa ikiongea bila utekelezaji suala ambalo linawakatisha
tamaa wananchi.
Akijibu malalamiko hayo Ofisa elimu sekondari,Anastazia Manumbu,
aliliambia baraza hilo kuwa bado halmashauri inaendelea na mchakato wa
ukamilishaji wa sekondari hiyo kwa kubainisha kwamba kwa kipindi hiki
wanaendelea na ujenzi wa vyoo na nyumba ya mwalimu.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kahama,Abel
Shija,alihitimisha mjadala na kuungwa mkono na madiwani wote kwa kumtaka
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo,Kapami,kuhakikisha
Sekondari hiyo,inakamilika mapema iwezekanavyo, kwa kutumia mafungu ya
dharura iwapo kama haikupangiwa bajeti.