KUREJEA KUNDINI KWA BANDA KWAONGEZA MATUMAINI YA ULINZI KWA OMOG
Baada
ya beki Abdi Banda kurejea katika kikosini kumeongeza matumaini kwa
Kocha Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog ya kuwaondoa wapinzani Azam
FC watakaopambana nao Jumamosi hii kwenye mechi ya Kombe la FA hatua ya
nusu fainali.
Banda
amerejea kikosini hivi karibuni akitoka kifungoni baada ya Kamati ya
Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirisho la Soka Tanzania (TFF)
kumfutia adhabu kwa kosa la kumpiga ngumi kiungo wa Kagera Sugar, George
Kavila.
Awali,
Banda alisimamishwa na Kamati ya Saa 72 ya shirikisho ambapo aliikosa
michezo miwili ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbao FC na Toto Africans kwenye
Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Omog
alisema kuwa anafurahi kuona beki wake ambaye ni tegemeo akirejea
uwanjani kwenye mechi dhidi ya Azam baada adhabu yake kufutwa.
Omog
alisema, kwenye mechi mbili ambazo beki huyo hakuwepo pengo lake
lilionekana kutokana na umuhimu wake mkubwa kwenye kikosi chake
kilichopanga kuchukua mataji mawili ya ligi kuu na Kombe la FA.
“Sina
hofu na kikosi changu kuelekea mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA
tutakapokutana na Azam Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Taifa, kwani nina
furaha ya kurejea kwa Banda.
“Kama
unavyojua Banda alikosa michezo miwili ya ligi kuu dhidi ya Mbao
tuliowafunga mabao 3-2 na Toto African ambayo tulitoka suluhu, hivyo
nina imani kubwa ya kupata ushindi kwenye mchezo huo.
“Ninafahamu
mechi itakuwa mgumu sana, lakini kwa upande wetu Simba tumejiandaa vema
kwa ajili ya mchezo huo na tayari tumeziboresha baadhi ya nafasi zenye
upungufu kuhakikisha tunavuka kisiki hiki cha kwanza tukisubiria ligi
kuu,” alisema Omog.