EfG YAPONGEZWA KUFUNGUA KLABU ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA SOKO LA ILALA BOMA JIJINI DAR ES SALAAM.
Mfanyabiashara wa nguo za mitumba ya
kike katika Soko la Ilala Boma jijini Dar es Salaam, Daud Omary
(kushoto), akitoa maelezo Dar es Salaa jana ya vitendo vya ukatili wa
kijinsia wanavyofanyiwa na baadhi ya askari polisi wa Kituo cha Pangani
kwa Mwezeshaji wa kisheria katika soko hilo (kulia) kutoka Shirika la
Equality for Growth (EfG), wakati wa uhamsishaji wa kufungua klabu za
mabadiliko ya kupinga ukatili wa kijinsia masokoni unaofanywa na Shirika
hilo kwa kusimamiwa na Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake
Tanzania (WLAC) kupitia kampeni ya miezi miwili ya Tunaweza. Katikati
ni mfanyabiashara Seleman Adam.
Fundi ushonaji nguo katika Soko la
Ilala Boma, Abdallah Omari (kulia), akitoa maelezo kwa mwezeshaji sheria
kutoka Shirika la EfG, Aisha Juma wakati wa kujiunga na klabu ya
mabadiliko ya wapinga ukatili wa kijinsia.
Fundi ushonaji nguo
katika Soko la Ilala Boma, Hamisi Bweni (kulia), akitoa maelezo kwa
mwezeshaji sheria kutoka Shirika la EfG, Aisha Juma wakati wa kujiunga
na klabu ya mabadiliko ya wapinga ukatili wa kijinsia.
Mama Lishe, Zaina Amri (kushoto), akijieleza kwa mwezeshaji wa sheria, Irene Daniel, wakati akijiunga na klabu hiyo.
Wafanyabiashara katika soko hilo
wakijiunga na klabu hiyo. Kutoka kulia ni Fatuma Bayuni, Ibrahim Said na
kushoto ni mwezeshaji wa kisheria Irene Daniel kutoka EfG.
Mama Lishe Sauda Mwinyi akisoma kipeperushi kabla ya
kujiunga na klabu ya mabadiliko.
Mama Lishe Wanamabadiliko wakiweka bango la kupinga ukatili huo. Kulia ni Fatuma Bayuni na Zaina Amri.
Mwezeshaji wa Kisheria masokoni, Irene
Daniel (kulia), pamoja na wanamabadiliko wa Soko la Ilala Boma,
wakionesha vipeperushi vya kupinga ukatili wa kijinsia masokoni. Kutoka
kushoto ni Zaina Amri, Ibrahim Saidi na Fatuma Bayuni.
Na Dotto Mwaibale
WAFANYABIASHARA katika Soko la Ilala
Boma jijini Dar es Salaam wamelipongeza Shirika la Equality for Growth
(EfG) kwa kuwahamasisha kufungua klabu za kupinga ukatili wa kijinsia
masokoni.
Wakizungumza na waandishi wa habari Dar
es Salaam jana, walisema kufunguliwa kwa klabu hizo kutawasaidia kwa
karibu kukabiliana na vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia
vinavyofanyika katika soko hilo na mengine.
"Binafsi nalipongeza shirika hili kwa
hatua hii nzuri waliofikia ya kutuhamasisha kuwa mabalozi wa kupinga
vitendo vya ukatili wa kijinsia na kutusogezea huduma hii karibu ambayo
itapunguza kama sio kumaliza kabisa vitendo vya ukatili masokoni"
alisema Abdallah Omari ambaye ni mshonaji nguo katika soko hilo.
Omari alisema changamoto kubwa
waliyokuwa nayo ni wapi walipaswa kutoa taarifa za ukatili huo wa
kijinsia kwani wengi wao walikuwa hawajui lakini kwa kuanzishwa klabu
hizo na kuwa na namba za wawezeshaji wa kisheria kwao milango ya utoaji
wa taarifa hizo sasa imefunguliwa.
Mfanyabiashara wa kuuza nguo za mitumba
za kike katika soko hilo, Daud Omari alisema kuna baadhi ya polisi
kutoka kituo cha Pangani wamekuwa wakiwafanyia ukatili wa kijinsia pale
wanapoenda kuwakamata na kuanza kuwapiga na kibaya zaidi wanakuwa
hawajitambulishi mpaka wanapofika kituoni.
"Unajua hapa sokoni kunakuwa na mambo
mengi hasa pale tunapopishana na wenzetu na kwenda kushitaki polisi
wakifika wao uanza kupiga watu bila ya kujitambulisha na ukifika polisi
ndipo wanajitambulisha kuwa wao ni polisi kitendo hicho kwetu tunahesabu
kuwa ni ukatili wa kijinsia tunaofanyiwa na askari hao" alisema Omari.
Omari Lubuva mfanya biashara katika eneo
hilo alisema mtu anapotoa oda ya chakula kwa mama lishe akipelekewa
anapo muambia mama lishe husika kuwa ondoka na chakula chako
umekichelewesha nimemuagiza mwingine aniletee huo ni ukatili wa kijinsia
dhidi ya mama lishe.
Aliwaomba wafanyabiashara wenzake wenye tabia hiyo kuacha kufanya hivyo kwani jambo hilo ni ukatili mbaya kwa mama lishe hao.
Seleman Adam aliwapongeza EfG kwa hatua
walioifikia ya kuwasogezea huduma hiyo kwa mara nyingine hivyo akayaomba
mashirika mengine kujitokeza kusaidia wananchi katika maeneo mengine
kwani katika jamii kuna changamoto nyingi.
Mwanasheria wa Shirika hilo, Muna
Abdallah alisema muitikio wa kufungua klabu za mabadiliko za kupinga
ukatili wa kijinsia katika masoko waliyoyatembelea ni mkubwa mno.
"Kwa kweli watu wengi wameonesha
kuchoshwa na vitendo hivyo na wamepokea kwa mikono miwili mradi huu
tuliouanzisha wa kufungua klabu za mabadiliko za kupinga ukatili wa
kijinsia masokono" alisema Abdallah.
Mratibu wa mradi huo ambaye pia ni
Mwanasheria wa Shirika hilo, Mussa Mlawa alisema msimamizi mkuu wa mradi
huo kupitia kampeni ya Tunaweza ni Kituo cha Msaada wa Sheria kwa
Wanawake Tanzania (WLAC) lakini EfG wao wanaiendesha kampeni hiyo ya
miezi miwili katika masoko matano yaliyopo jijini Dar es Salaam ambayo
ni Ilala Boma, Ferry, Mchikichini, Temeke Sterio na Buguruni.
Alisema lengo kubwa la mradi huo ni kuwa
na wanamabadiliko masokoni ambao watasaidia kupambana na vitendo hivyo
si katika maeneo ya masoko pekee bali hata majumbani kwa jamii.